
Mawakili Nicholas Mugarura, Mwesigwa Muhingo na David Saire Manoti, wanaomwakilisha mmoja kati ya watoto wa marehemu Mchungaji Getrude Rwakatare wametoa taarifa kuhusu mgogoro wa mirathi ya marehemu.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa mawakili hao, David Saire Manoti, amesema marehemu Mchungaji Rwakatare alikuwa kiongozi maarufu wa Kanisa la Assemblies of God, Mikocheni B, Mlima wa Moto, pamoja na kuwa Mbunge wa Kuteuliwa na Rais.
Amesema baada ya kifo cha mama Rwakatare aliyefariki dunia Aprili 20, 2020, Shauri la Mirathi Na. 32 la mwaka 2020 lilifunguliwa katika Mahakama Kuu ya Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa Mahakama Kuu, Kituo Jumuishi cha Haki Temeke.
Katika shauri hilo, watoto wa marehemu waliteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi.
Manoti amesema marehemu Mchungaji Rwakatare alikuwa akimiliki shule kadhaa ambazo, kupitia hati maalum ya ugawaji wa mali za mirathi (Accounts of Estate) ya Novemba 26, 2024, na baada ya kuidhinishwa na Mahakama Kuu, ziligawanywa kwa watoto wake.
Amesema kila mtoto aligawiwa shule tatu. Hata hivyo, kwa upande wa mtoto mmoja, Tibe Kenneth Rwakatare, utekelezaji wa ugawaji huo umekumbana na changamoto kubwa na kuonya kuwa watu wasinunue mali za marehemu mpaka ufumbuzi wa utata huo utakapopatikana.