
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, amesema chama hicho hakitakuwa tayari kushiriki katika mazungumzo yoyote iwapo Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, ataendelea kuwa gerezani.
Heche ameyasema hayo leo, Agosti 29, 2026, katika Kikao Maalumu cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika katika Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Amesema msimamo wa chama ni kwamba Lissu, ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya uhaini, ndiye anayebeba dira ya CHADEMA na hivyo anapaswa kuwa sehemu inayoongoza aina yoyote ya mazungumzo yatakayofanyika.

Heche amesema CHADEMA haiwezi kuingia katika mazungumzo chini ya vitisho au kushurutishwa, akisisitiza kuwa viongozi wa chama hicho hawako tayari kushiriki mazungumzo kwa kulazimishwa.
Aidha, amesema viongozi wa CHADEMA wanaoshikiliwa kwa makosa ambayo ameyataja kuwa ni “uongo” wanapaswa kuachiliwa, huku akitaka kupatikana kwa msuluhishi wa kitaifa au kimataifa anayeaminika ili kusaidia kuwakutanisha wahusika na kuwezesha mchakato wa mazungumzo.

CHADEMA yaahirisha Baraza Kuu
Katika kikao hicho, Kamati Kuu ya CHADEMA imeazimia kuahirisha kikao cha Baraza Kuu la chama hicho kilichokuwa kifanyike Septemba 15, 2026.
Naibu Katibu Mkuu Bara wa CHADEMA, Amani Golugwa, amesema uamuzi huo umetolewa baada ya Kamati Kuu kujadili, miongoni mwa mambo mengine, maandalizi ya Baraza Kuu pamoja na mwenendo wa kesi inayomkabili Lissu.
Golugwa amesema tarehe mpya ya kufanyika kwa kikao hicho bado haijawekwa na itapangwa baadaye.
Kamati Kuu yaweka nguvu kwenye kesi ya Lissu
Kuhusu kesi hiyo, Kamati Kuu imewaelekeza viongozi wakuu wa chama kuelekeza nguvu katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kesi hiyo.
Pia, CHADEMA imesema itaendelea kuongeza nguvu katika madai yake ya Katiba Mpya, sambamba na kuendelea kushinikiza kuachiwa kwa Mwenyekiti wake, ikisisitiza msimamo wa chama kuwa Lissu hana hatia.
CHADEMA yakusanya Sh milioni 302
Katika kikao hicho, Kamati Kuu pia imepokea taarifa kuhusu kampeni ya uchangishaji fedha ya “Tone kwa Tone” kuelekea Baraza Kuu la chama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa kwenye kikao hicho, jumla ya Sh milioni 302 zimekusanywa kupitia zoezi hilo.
Kamati Kuu imewapongeza na kuwashukuru wanachama wote walioshiriki katika uchangishaji huo.