×

Video: Rais Samia Atoa Agizo Zito kwa Mnyeti Kuhusu Madini ya Katoro

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, kusimamia kwa karibu shughuli za uchimbaji na biashara ya madini, hususan katika Mji wa Katoro, ili kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki kupitia ulipaji wa kodi.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo, Septemba 2, 2026, wakati akizungumza katika Ikulu ya Tunguu, Zanzibar, akimtaka Mnyeti kuhakikisha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wanaendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu.

Amesema mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali yamewezesha wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa ufanisi na wananchi kunufaika na rasilimali za madini.

Akizungumza kuhusu hali ya Katoro, Rais Samia amesema utajiri unaopatikana katika eneo hilo unapaswa kuambatana na ulipaji wa kodi na kuchangia maendeleo ya Mkoa wa Geita.

“Unayoyasikia Katoro ni kwa sababu tumejenga mazingira mazuri, wachimbaji wadogo wanachimba vizuri, watu wamenufaika, utajiri umepatikana wa kutosha. Sijakupeleka ukajitajirishe; kasimamie wanaotajirika, walipe kodi zetu, waendelee kufanya kazi zao na mkoa upate maendeleo,” amesema.

Rais Samia pia amemtaka Mnyeti kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuhakikisha urafiki au mahusiano binafsi hayaathiri utekelezaji wa majukumu yake ya kiuongozi.

Amesema Mnyeti anaifahamu Geita kutokana na uzoefu wake wa awali katika eneo hilo, lakini ametakiwa kutenganisha masuala ya kikazi na mahusiano binafsi.

“Kwa hiyo, nenda kasimamie vyema. Najua pale wewe si mgeni, ni mwenyeji, sasa vile vijiji vyako ulivyokuwa navyo huko nyuma, nataka uachane navyo ila usiache marafiki, lakini usiwa-entertain kwenye kazi yako,” ameongeza Rais Samia.

Kauli hiyo ya Rais inalenga kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na kuhakikisha utajiri unaopatikana kupitia uchimbaji unaleta manufaa mapana kwa wachimbaji, wafanyabiashara, Serikali na wananchi.

Aidha, msisitizo wa ulipaji kodi unalenga kuhakikisha mapato yatokanayo na shughuli za madini yanatumika katika kugharamia huduma na miradi ya maendeleo, hususan katika Mkoa wa Geita ambao ni miongoni mwa maeneo yenye shughuli kubwa za uchimbaji wa madini nchini.

Stori na Lailath Burhan | GPL – TUDACO

Leave a Comment