×

Joheirry Mola Aibuka Mshindi wa Miss World 2026 nchini Vietnam

Mshiriki kutoka Dominican Republic, Joheirry Mola, ametangazwa kuwa mshindi wa mashindano ya Miss World 2026, yaliyofanyika nchini Vietnam na kufikia kilele chake usiku wa kuamkia leo Jumapili, Septemba 6, 2026.

Miss World 2026 kutoka Dominican Republic, Joheirry Mola.

Mola ametwaa taji hilo katika fainali ya 73 ya mashindano hayo ya kimataifa, akiwashinda washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani waliokusanyika Vietnam kuwania taji hilo.

Katika nafasi ya pili alimaliza Elisabeth Reynes wa Hispania, huku Taanusiya Chetty wa Malaysia akishika nafasi ya tatu.

Tukio hilo pia lilihudhuriwa na mshindi wa Miss World 2025, Suchata Chuangsri wa Thailand, ambaye alikabidhi taji hilo kwa Mola, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kukabidhi taji kwa mshindi mpya.

“Nina furaha isiyo na kifani na bado ninajaribu kuamini kilichotokea. Nina furaha sana, na ningependa kuona nchi yangu ikisherehekea ushindi huu kwa sasa. Wanastahili furaha hii! Siwezi kusubiri kuona yaliyo mbele yangu, niko tayari.”

Hayo ni maneno ya Miss World 2026, Joheirry Mola wa Dominican Republic, baada ya kutwaa taji hilo katika fainali ya mashindano hayo yaliyofanyika nchini Vietnam.

 

Leave a Comment