×

Shahidi wa Nne Kesi ya Uhaini Lissu Kuendelea Kutoa Ushahidi leo

Dar es Salaam: Shahidi wa nne katika kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia, leo Septemba 8, 2026 anaendelea kutoa ushahidi wa utetezi dhidi ya Lissu.

Jana, Septemba 7, 2026, Rupia alianza kutoa ushahidi wake ambapo Lissu alimhoji kuhusu mkutano uliofanyika Aprili 3, 2025, ukiwemo ulikuwa na lengo gani na nani aliyeandaa mkutano huo.

Katika majibu yake, Rupia alieleza kuwa mkutano huo ulilenga kuwakutanisha watia nia wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa ajili ya kujadili msimamo wa chama wa “No Reforms, No Election”.

Alisema uamuzi wa kufanyika kwa mkutano huo ulifanywa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, pamoja na Sekretarieti ya chama, akisisitiza kuwa mkutano huo haukuandaliwa na Tundu Lissu kama inavyodaiwa.

Rupia pia alieleza kuwa Kurugenzi ya Mawasiliano na Uenezi chini yake ndiyo iliyohusika na kuandaa taarifa kwa umma pamoja na kuwaalika waandishi wa habari kuhudhuria mkutano huo.

Hata hivyo, alisema waandishi wa habari walioalikwa hawakupewa maelekezo yoyote ya kikazi wala kuagizwa kurusha matangazo ya moja kwa moja kutoka katika mkutano huo.

Katika ushahidi wake, Rupia alisisitiza kuwa Lissu alihudhuria mkutano huo kama mzungumzaji mkuu kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, na kwamba hakuhusika katika ualikaji wa vyombo vya habari.

Aidha, shahidi huyo alieleza kuwa umiliki wa maudhui yote ya habari yaliyorekodiwa siku hiyo ulikuwa chini ya vyombo vya habari vilivyohudhuria, na si CHADEMA au viongozi wake.

Leave a Comment