
CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT) kimesema, kimepokea taarifa kuhusu tukio lililotokea Septemba 8, 2026 katika eneo la Lugalo, Kinondoni jijini Dar es Salaam, linalomhusisha Dkt.Conrad Agonza Kahyoza ambaye ni Daktari Bingwa Magonjwa ya Ndani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila na Askari wa Usalama Barabarani mwenye namba F.8886 SGT.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 8,2026 na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt.Alex Elifuraha Msoka.
Dkt.Msoka amesema,baada ya tukio hilo, uongozi wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) umefanya mazungumzo na Jeshi la Polisi Tanzania kupitia Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Murilo Jumanne Muliro, na kufahamishwa kwamba Dkt.Agonza alipata majeraha na kupelekwa haraka hospitalini kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya dharura na hali yake imeimarika.

Aidha,kwa sasa anashikiliwa katika kituo cha Polisi Oysterbay na taratibu za kisheria zinaendelea.
“Chama cha Madaktari Tanzania kinasisitiza yafuatayo kwanza, kwa kuzingatia hali ya Dkt. Agonza na mahitaji yake ya matibabu,MAT inaendelea kufuatilia kwa karibu ustawi wake na kuhakikisha kwamba anapata huduma stahiki za matibabu kwa wakati wowote atakapohitaji.”
Pili,amesema uongozi wa MAT kupitia wanasheria wake unaendelea kufuatilia taratibu za kisheria kuhakikisha anapata msaada wa kisheria wa haraka ikiwa ni pamoja na dhamana.
Tatu, amesema MAT kwa kushirikiana muajiri wa Dkt.Agonza ambaye ni Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila pamoja na familia itaendelea kufuatilia na kutoa taarifa kulingana na mwenendo wa shauri hili.
“Chama cha Madaktari Tanzania kinaendelea kufuatilia suala hili kwa karibu na kitaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika kwa mamlaka husika, huku kikilinda maslahi, utu na haki za mwanachama wake kwa mujibu wa sheria.”
