×

Misri Yaitaka Iran Kusitisha Mashambulizi Dhidi Ya Nchi za Kiarabu

Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi, ameitaka Iran kuchukua hatua za kupunguza mvutano unaoongezeka katika Mashariki ya Kati na kushirikiana katika kutafuta suluhisho la kudumu la amani.

El-Sisi ametoa wito huo Jumapili, Septemba 14, 2026, wakati wa mazungumzo na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa BRICS mjini New Delhi, India.

Katika mazungumzo hayo, El-Sisi pia ameitaka Iran kusitisha mashambulizi dhidi ya mataifa ya Kiarabu, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu uhusiano mwema kati ya nchi hizo pamoja na mamlaka na uhuru wa mataifa ya eneo hilo.

Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya Misri, Mohamed El-Shennawy, El-Sisi ameitaka Tehran kufanya “juhudi zote zinazowezekana” kupunguza mvutano, huku akisisitiza kuwa Misri inaendelea kuunga mkono juhudi za kurejesha utulivu katika eneo hilo.

Misri imeongeza juhudi zake za kidiplomasia katika kutafuta njia ya kumaliza mzozo huo na kufufua mazungumzo yaliyokwama kati ya Iran na Marekani.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, ametoa wito wa kurejea kwenye mazungumzo ya Marekani na Iran, akisema suluhisho la kidiplomasia linapaswa kupewa kipaumbele ili kuzuia mzozo huo kuenea zaidi.

Mvutano umeendelea pia kuzunguka Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa nishati ambayo kabla ya vita ilipitisha takribani moja ya tano ya mafuta yanayotumika duniani.

Oman inaongoza juhudi za kidiplomasia za kuwezesha usafiri kupitia njia hiyo, huku Iran na mataifa ya Ghuba yakitarajiwa kufanya mazungumzo mjini Muscat Jumatatu. Hata hivyo, afisa mmoja wa Iran amesema hakuna makubaliano ya mwisho yanayotarajiwa kusainiwa kuhusu Mlango wa Hormuz katika mkutano huo.

Mkutano wa El-Sisi na Pezeshkian umefanyika wakati mzozo wa Mashariki ya Kati ukiwa miongoni mwa masuala makuu yaliyojadiliwa katika mkutano wa siku mbili wa BRICS.

Viongozi wa BRICS walipitisha tamko la pamoja Jumamosi wakieleza “wasiwasi mkubwa” kuhusu kuongezeka kwa mzozo huo na kutoa wito wa “kujizuia kwa kiwango cha juu” pamoja na kutatua migogoro kupitia mazungumzo na diplomasia.

Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ziliunga mkono tamko hilo licha ya kuwa na misimamo tofauti kuhusu mzozo huo.

Kwa upande mwingine, Pezeshkian alifanya mazungumzo ya ana kwa ana na Mwanamfalme wa Abu Dhabi, Sheikh Khaled bin Mohamed bin Zayed Al-Nahyan. Mazungumzo hayo yameelezwa kuwa ya kiwango cha juu zaidi kati ya Iran na UAE tangu kuanza kwa mzozo huo.

Viongozi hao walijadili namna ya kupunguza mvutano wa kikanda na kuimarisha usalama na utulivu, huku Sheikh Khaled akisisitiza umuhimu wa mazungumzo na suluhisho la kidiplomasia.

Misri, Iran na UAE ni miongoni mwa wanachama wapya wa BRICS iliyopanuliwa. Misri, Ethiopia, Iran na UAE zilijiunga mwaka 2024, zikifuatiwa na Indonesia mwaka 2025.

Kwa sasa, BRICS inawakilisha zaidi ya asilimia 40 ya watu duniani na takribani robo ya uchumi wa dunia, huku ikilenga kuongeza ushawishi wa nchi zinazoibukia katika taasisi za kimataifa na kukuza mfumo wa dunia wenye nguvu nyingi za kisiasa na kiuchumi.

Mkutano wa New Delhi umeweka mkazo mkubwa katika nafasi ambayo BRICS inaweza kuchukua katika juhudi za kidiplomasia, huku Rais wa China, Xi Jinping, akizitaka nchi wanachama wa BRICS kusaidia kuendeleza suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Mashariki ya Kati.

Leave a Comment