UVINZA, KIGOMA — Mahakama ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Rajabu Uhuru (36), dereva wa bodaboda na mkazi wa Kijiji cha Ilalangulu, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13.
Hukumu hiyo imetolewa Septemba 17, 2026 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Uvinza, Misana Majula.
Katika hukumu hiyo, Hakimu Majula amesema Mahakama imejiridhisha bila kuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo, kutokana na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, tukio hilo lilitokea Juni 12, 2026, majira ya saa 3 usiku, katika eneo la Kigulwe, Kijiji cha Ilalangulu, Kata ya Mtego wa Noti, Tarafa ya Nguruka, Wilaya ya Uvinza.
Mahakama ilielezwa kuwa baada ya kutenda kosa hilo, mshtakiwa alikimbilia jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujificha na kukwepa mkono wa sheria.
Hata hivyo, alikamatwa baada ya Jeshi la Polisi kufanya msako uliomwezesha kunaswa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Majula amesema adhabu hiyo ni fundisho kwa wengine na sehemu ya juhudi za Serikali katika kulinda haki na usalama wa watoto pamoja na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mahakama imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaokiuka haki na usalama wa watoto.
Stori na Mwajabu Abdallah | GPL -TUDACO