×

Yas Yafungua Duka Jipya Kahama, Yaongeza Fursa za Huduma na Ajira

Kahama, Septemba 24, 2026 — Wakazi na wafanyabiashara wa Kahama, mkoani Shinyanga, wamepata fursa zaidi ya kupata huduma za mawasiliano na kifedha kwa urahisi baada ya

Akizungumza katika uzinduzi wa duka hilo, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mhe. Mataluma Kaniki, amesema uwekezaji wa sekta binafsi una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa eneo hilo na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Amesema Kahama inaendelea kukua kwa kasi kutokana na shughuli za madini, kilimo na biashara, hivyo uwekezaji wa kampuni binafsi unasaidia kuongeza huduma pamoja na shughuli za kiuchumi zinazozunguka uwekezaji huo.

“Kahama ni miongoni mwa maeneo yanayokua kwa kasi kiuchumi kutokana na shughuli za madini, kilimo na biashara. Tunapopata uwekezaji kama huu, tunaona matokeo yake si katika huduma pekee, bali pia katika ajira, biashara zinazozunguka uwekezaji huo na mchango wake katika uchumi wa Manispaa yetu,” amesema Kaniki.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha uwekezaji zaidi kufanyika Kahama.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Uendeshaji wa Yas Tanzania, Bi. Mwangaza Matotola, amesema duka hilo limefunguliwa kwa lengo la kuwasogezea huduma karibu wakazi wa Kahama na kuwapa sehemu ya kupata msaada pale wanapohitaji.

“Tunataka mteja wa Kahama apate huduma anayoihitaji kwa urahisi na kwa wakati. Duka hili linatupa nafasi ya kuwa karibu zaidi na wateja wetu, kusikiliza mahitaji yao, kutatua changamoto zao na kuwapatia huduma za Yas na Mixx katika sehemu moja,” amesema Matotola.

Kwa mujibu wa Matotola, duka hilo ni sehemu ya mtandao wa zaidi ya maduka 556 ya Yas yaliyopo nchini, ambayo yanawawezesha wateja kupata huduma mbalimbali zikiwemo laini, intaneti, vifaa vya mawasiliano pamoja na huduma za kifedha.

Amesema upanuzi wa vituo vya huduma unaenda sambamba na uwekezaji wa zaidi ya Sh trilioni moja ambao Yas imeufanya katika kupanua na kuboresha miundombinu na huduma zake nchini.

Matotola amesema Yas kwa sasa ina zaidi ya minara 4,900, inayowezesha huduma za teknolojia za 4G na 5G katika maeneo mbalimbali, huku kampuni hiyo ikihudumia zaidi ya wateja milioni 33.2 Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema uwekezaji huo unalenga kuhakikisha ukuaji wa matumizi ya huduma za kidijitali unaenda sambamba na upatikanaji wa huduma na msaada wa moja kwa moja kwa wateja.

“Kadiri matumizi ya teknolojia yanavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya wateja yanavyobadilika. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza si tu kwenye mtandao, bali pia kwenye maeneo ambayo mteja anaweza kufika, kuzungumza nasi na kupata suluhisho la mahitaji yake,” amesema.

Mbali na kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kifedha, kufunguliwa kwa duka hilo kumeongeza pia fursa za ajira kwa vijana wa Kahama, ikiwa ni miongoni mwa manufaa ya uwekezaji huo kwa jamii.

Leave a Comment