×

Wicknell Chivayo: Mfanyabiashara Aliyejenga Ukaribu na Viongozi wa Afrika

Mfanyabiashara wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, ambaye amefariki katika ajali ya helikopta nchini Zimbabwe pamoja na mkewe Lucy Muteke, alikuwa mmoja wa wafanyabiashara waliovutia hisia kutokana na maisha yake ya kifahari na ukaribu wake na viongozi mbalimbali barani Afrika.

Chivayo, aliyekuwa akijulikana kama Sir Wicknell, alijijengea umaarufu kupitia mitandao ya kijamii, ambako mara kwa mara alionyesha utajiri wake, magari ya kifahari, safari za kimataifa pamoja na zawadi kubwa alizokuwa akiwapatia watu mbalimbali.

Miongoni mwa waliowahi kunufaika na zawadi zake ni wanamuziki, waimbaji wa injili, wachezaji wa mpira, viongozi wa dini na watu wengine aliowaona kuwa wazalendo.

Maisha yake ya utajiri yaliambatana pia na maswali kuhusu chanzo cha fedha zake. Chivayo aliwahi kueleza kuwa biashara zake zilihusisha tenda za serikali pamoja na miradi ya nishati, uhandisi, ujenzi na umeme, akisema alifanya kazi na washirika kutoka nje ya Zimbabwe.

Kampuni yake, Intratrek Zimbabwe, iliwahi kuhusishwa na mkataba wa mradi wa nishati ya jua wa Gwanda wenye thamani ya takribani dola milioni 172.8 (ni takribani TSh 456.1 bilioni)

Mradi huo baadaye uliibua mzozo wa kisheria kuhusu utekelezaji wake, huku Chivayo na kampuni yake wakihusika katika kesi mbalimbali. Kwa mujibu wa BBC, baadaye alishinda kesi dhidi ya kampuni ya umeme ya Zimbabwe na akaondolewa katika mashtaka ya jinai yaliyohusishwa na suala hilo.

Historia yake pia ilihusisha kipindi cha kukaa gerezani, ambako alianzisha urafiki na Simon Mann, raia wa Uingereza aliyekuwa amefungwa nchini Zimbabwe baada ya kuhukumiwa katika kesi iliyohusishwa na njama ya mapinduzi.

Baada ya hapo, Chivayo aliendelea kujijenga katika biashara na kujitengenezea jina kubwa nchini Zimbabwe.

Alikuwa akijieleza kama mtu aliyejijenga mwenyewe, akieleza kuwa alikulia Chitungwiza katika mazingira magumu baada ya kumpoteza baba yake akiwa na umri mdogo.

Pamoja na biashara zake, Chivayo alijulikana pia kwa ukaribu wake na viongozi wa kisiasa. Kupitia mitandao yake ya kijamii, aliwahi kuchapisha picha akiwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe, Rais Emmerson Mnangagwa, pamoja na viongozi wengine wa Afrika.

Miongoni mwa viongozi wa Afrika ambao picha zao ziliwahi kuonekana kwenye akaunti zake ni Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Rais William Ruto wa Kenya na Rais Lazarus Chakwera wa Malawi.

Licha ya utajiri na umaarufu wake, Chivayo mara kwa mara alisisitiza kuwa hakuwa na nia ya kuingia kwenye siasa, akisema alijikita zaidi katika biashara na kujenga mafanikio yake.

Kifo chake katika ajali ya helikopta kimehitimisha maisha ya mfanyabiashara ambaye, kwa miaka kadhaa, alibaki kuwa mtu mwenye ushawishi na mjadala mkubwa nchini Zimbabwe na nje ya mipaka yake.

Leave a Comment