ZANZIBAR: Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imepokea cheti cha shukrani kwa mchango wake katika kufanikisha maonesho ya Tech & AI Expo Zanzibar 2026, yaliyowakutanisha wadau wa teknolojia, wabunifu na viongozi kujadili maendeleo ya uchumi wa kidijitali Zanzibar.
Cheti hicho kilikabidhiwa na Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga, na kupokelewa na Afisa Mkuu wa Yas Business, Norman Kiondo, katika hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika kuhitimisha maonesho hayo.
Waziri Soraga ameishukuru Yas kwa kuwa mdhamini mkuu wa tukio hilo, huku pia akitoa tuzo kwa washindi wa shindano la Hackathon pamoja na washiriki wa mijadala iliyofanyika wakati wa maonesho.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Soraga amesisitiza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuendelea kukuza ubunifu, teknolojia na matumizi ya akili bandia katika kuendeleza uchumi wa kidijitali.
Kwa upande wake, Norman Kiondo amesema Yas itaendelea kushirikiana na Serikali, sekta binafsi na wabunifu katika kuendeleza matumizi ya teknolojia Zanzibar.
“Tunashukuru kwa kutambuliwa kwa mchango wetu katika maonesho haya. Yas itaendelea kuwekeza katika miundombinu na huduma za kidijitali Zanzibar ili kuwasaidia wananchi na biashara kutumia teknolojia katika shughuli zao za kila siku,” amesema Kiondo.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wabunifu ni muhimu katika kuhakikisha teknolojia inatumika kama kichocheo cha maendeleo ya Zanzibar.
Maonesho ya Tech & AI Expo Zanzibar 2026 yamekuwa jukwaa la wadau kujadili fursa na changamoto zinazotokana na maendeleo ya teknolojia, ubunifu na matumizi ya akili bandia katika uchumi wa Zanzibar.
