×

Polisi Dodoma Yawakamata Watuhumiwa 98 Kwa Makosa Mbalimbali

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda raia na mali zao, ambapo katika kipindi cha mwezi Septemba 7 hadi Oktoba 7, 2026, limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 98 kwa makosa mbalimbali, akiwemo mtuhumiwa mmoja wa kosa la ubakaji wa mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 15.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, watuhumiwa 97 wanashikiliwa kwa makosa mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya, biashara ya bidhaa bandia pamoja na makosa mengine.

Katika operesheni hizo, Polisi wamekamata dawa za kulevya aina mbalimbali zikiwemo bangii, pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika katika uuzaji na matumizi ya dawa hizo. Vilevile, Polisi wamekamata bidhaa bandia zikiwemo betri za simu aina ya Itel, pikikipiki, televisheni, mitungi ya gesi, vipuri vya magari na vifaa vingine.

Aidha, watuhumiwa 30 wamekamatwa kwa makosa ya uvunjaji, huku watuhumiwa wanne wakikamatwa kwa makosa ya mauaji, na wengine wanne kwa kuharibu miundombinu ya barabara.

Jeshi hilo pia limewakamata watuhumiwa watano kwa makosa ya kuchoma moto nyumba pamoja na watuhumiwa 16 kwa makosa mbalimbali ya wizi, wakiwemo waliokutwa wakitumia pikipiki katika kutekeleza uhalifu.

Kwa upande wa usalama barabarani, Kikosi cha Usalama Barabarani kimefanikiwa kudhibiti ajali za barabarani kwa kukamata makosa 13,185 na kufungia leseni za madereva 10 kwa muda wa miezi mitatu. Hatua hiyo imechukuliwa sambamba na kudhibiti ajali za barabarani na kuhakikisha madereva wanaendesha kwa mwendo kasi unaokubalika.

Kwa upande wa mashauri ya Mahakamani, jumla ya washitakiwa 13 wamehukumiwa vifungo mbalimbali kutokana na makosa tofauti yaliyotendwa. Hukumu hizo ni pamoja na kifungo cha miaka 30, kulipa faini ya Sh milioni moja, kifungo cha miezi 12, kifungo cha mwaka mmoja, kifungo cha miezi sita na kulipa faini ya Sh300,000.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limeendelea kuwasihi wananchi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa. Aidha, wananchi wametakiwa kutii sheria na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha Mkoa wa Dodoma unaendelea kuwa salama.

Leave a Comment