×

Billboard Yaitangaza Despacito Kuwa Wimbo Bora wa Wakati Wote

Wimbo wa “Despacito” wa Luis Fonsi na Daddy Yankee, akimshirikisha Justin Bieber, umeongoza orodha ya nyimbo bora za Latin za wakati wote iliyotolewa na jarida maarufu la muziki la Billboard, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 ya chati ya Hot Latin Songs.

Orodha hiyo inaangazia nyimbo zilizofanya vizuri zaidi katika historia ya chati hiyo kuanzia Oktoba 4, 1986 hadi Septemba 26, 2026, ikizingatia mafanikio ya nyimbo katika nafasi mbalimbali na muda zilizokaa kwenye chati.

Mafanikio hayo yanaimarisha nafasi ya “Despacito” katika historia ya muziki wa Latin, baada ya wimbo huo kutawala chati ya Hot Latin Songs kwa jumla ya wiki 56 kati ya mwaka 2017 na 2018.

Wimbo huo ulipata umaarufu mkubwa duniani, huku toleo la remix lililomshirikisha Justin Bieber likisaidia kuutambulisha zaidi kwa wasikilizaji ambao hawakuwa sehemu ya soko la muziki wa lugha ya Kihispania.

Katika orodha hiyo, nafasi ya pili imechukuliwa na “Propuesta Indecente” ya Romeo Santos, huku “DTMF” ya Bad Bunny ikishika nafasi ya tatu.

Nafasi ya nne imekwenda kwa “DÁKITI” ya Bad Bunny akishirikiana na Jhay Cortez, wakati “A Puro Dolor” ya Son by Four imekamilisha tano bora.

Nyimbo nyingine zilizoingia katika kumi bora ni “Si Tú Supieras” ya Alejandro Fernández iliyoshika nafasi ya sita, “RITMO (Bad Boys for Life)” ya Black Eyed Peas na J Balvin iliyokamata nafasi ya saba, pamoja na “No Me Doy Por Vencido” ya Luis Fonsi iliyoshika nafasi ya nane.

“El Perdón” ya Nicky Jam na Enrique Iglesias imechukua nafasi ya tisa, huku “Me Porto Bonito” ya Bad Bunny na Chencho Corleone ikikamilisha orodha ya nyimbo 10 bora.

Kwa upande wa wasanii, Bad Bunny ameongoza orodha ya wasanii bora wa Hot Latin Songs wa wakati wote. Nguvu yake katika chati hiyo inaonekana pia kupitia nyimbo tatu zilizoingia katika kumi bora, ambazo ni “DTMF”, “DÁKITI” na “Me Porto Bonito”.

Luis Fonsi naye ameonesha mafanikio makubwa katika orodha hiyo kupitia nyimbo mbili, “Despacito” na “No Me Doy Por Vencido”, zinazothibitisha mwendelezo wa mafanikio yake katika muziki wa Latin.

Orodha hiyo ya kihistoria inaangazia mchango wa wasanii na nyimbo mbalimbali katika kukuza muziki wa Latin kwa miongo minne, huku “Despacito” ikiendelea kuwa miongoni mwa nyimbo zilizovuka mipaka ya lugha na kufikia hadhira kubwa duniani.

Leave a Comment