×

Mtuhumiwa wa Bangi Kilo 23.63 Afungwa Miaka 30 Jela, Mwenzake Aachiwa Huru

MWANZA — Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza imemhukumu Corona Denis Matata (56) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukutwa na bangi yenye uzito wa kilogramu 23.63, huku mshtakiwa mwenzake akiachiliwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Corona alikamatwa Februari 26, 2026, katika eneo la Ihumilo, Luchelele, mkoani Mwanza, baada ya maafisa wa mamlaka hiyo kufanya upekuzi na kukamata bangi iliyokuwa imehifadhiwa kwenye mifuko mbalimbali.

Katika upekuzi huo, pia zilikamatwa kete 154 za bangi, kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Hukumu hiyo ilitolewa Septemba 25, 2026, ambapo Mahakama ilimwachia huru Kaua Raphael Rwechungura (36), aliyekuwa mshtakiwa wa pili, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kosa dhidi yake.

Aidha, Mahakama iliamuru bangi iliyokamatwa iteketezwe, huku simu mbili na fedha taslimu Sh215,000 zilizokamatwa zikiagizwa kurejeshwa kwa wamiliki wake.

Leave a Comment