×

Uwanja wa Gofu Wakamilika Serengeti, Kuzinduliwa Oktoba 18

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limekamilisha kwa asilimia 100 ujenzi wa Uwanja wa Gofu wa Fort Ikoma, uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, mkoani Mara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza utalii na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa la utalii wa kifahari.

Uwanja huo, unaojulikana kama Serengeti National Park Golf Course, unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Oktoba 18, 2026, na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji. Katika uzinduzi huo, wachezaji 81 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Malawi wanatarajiwa kushiriki mashindano ya gofu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TANAPA Oktoba 14, 2026, mradi huo ulizinduliwa rasmi Desemba 29, 2022, chini ya uongozi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa TANAPA, Jenerali mstaafu George Waitara, ukiwa na lengo la kupanua aina za shughuli za utalii, kuongeza muda wa kukaa kwa wageni na kuimarisha fursa za mapato yatokanayo na utalii.

Uwanja huo umejengwa katika eneo lenye ukubwa wa ekari 450, ukiwa na mashimo 18 yenye jumla ya par 72. Umegawanywa katika sehemu mbili, kila moja ikiwa na mashimo tisa. Uwanja huo una urefu wa kilomita 7.097, huku eneo lake likiwa na mandhari ya asili yanayowapa wageni fursa ya kucheza gofu huku wakifurahia mazingira ya Serengeti.

Aidha, mradi huo umejumuisha miundombinu mbalimbali, ikiwemo maeneo ya kuchezea na kufanya mazoezi, jengo la huduma kwa wachezaji (clubhouse), barabara, mifumo ya maji na umeme, pamoja na miundombinu ya umwagiliaji na mabwawa ya kuhifadhi maji. Miti ya asili 4,000 pia imepandwa katika eneo hilo kwa lengo la kuboresha uoto na mandhari.

Akizungumzia mradi huo, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Gibril Mwishawa, amesema uwanja huo ni sehemu ya juhudi za kubuni bidhaa mpya za utalii, kuongeza thamani ya vivutio vya hifadhi za taifa na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masoko ya kimataifa ya utalii.

Uwanja huo unatarajiwa kuvutia wapenzi wa gofu na watalii wanaotafuta uzoefu wa kipekee, sambamba na kufungua fursa mpya za ajira, biashara, usafiri, malazi, chakula na huduma nyingine kwa jamii zinazozunguka hifadhi hiyo.

TANAPA imesisitiza kuwa uhifadhi utaendelea kuwa kipaumbele katika utekelezaji na uendeshaji wa mradi huo. Tathmini ya athari kwa mazingira ilifanyika kabla ya ujenzi, huku usanifu ukizingatia mapito ya wanyamapori, kuepusha maeneo nyeti ya uhamaji wa nyumbu na kulinda mifumo muhimu ya ikolojia.

Hifadhi ya Taifa Serengeti ni miongoni mwa maeneo maarufu duniani kwa utajiri wa wanyamapori, mandhari ya kipekee na uhamaji mkubwa wa nyumbu, unaokadiriwa kuhusisha takribani wanyama milioni 1.5, pamoja na pundamilia na swala.

TANAPA inaamini kuwa uwepo wa uwanja huo utaongeza mvuto wa Serengeti, kupanua wigo wa shughuli za utalii na kuchochea ukuaji wa uchumi, huku urithi wa asili wa Tanzania ukiendelea kulindwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Leave a Comment