RIYADH: Waziri wa Ulinzi wa Sudan, Jenerali Hassan Kabroun, amelaani vikali mashambulizi yanayohusishwa na waasi wa Houthi dhidi ya Saudi Arabia, akiyataja kuwa ni vitendo vya kikatili na vya uhalifu.
Kabroun amesema shambulio lolote dhidi ya Saudi Arabia ni pigo kwa maeneo matakatifu ya Kiislamu na Waislamu duniani, akisisitiza kuwa serikali na wananchi wa Sudan wanalaani vitendo vyote vya Houthi dhidi ya Ufalme huo.
Kauli hiyo imekuja kufuatia taarifa ya shambulio la Jumamosi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Khalid, jijini Riyadh, ambalo kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Arab News, lilisababisha vifo vya watu 13, akiwemo raia mmoja wa Sudan, huku wengine 309 wakijeruhiwa.
Akizungumza Kabroun amelaani mashambulizi dhidi ya maeneo ya kiraia na malengo ya kijeshi, huku akiwakosoa wote wanaodaiwa kuwaunga mkono waasi wa Houthi.
Amesema Sudan inasimama pamoja na Saudi Arabia katika kukabiliana na vitisho vinavyoweza kuhatarisha usalama wa kikanda, akisisitiza mshikamano wa nchi hizo mbili dhidi ya kile alichokiita maadui wa Uislamu na ubinadamu.
Kauli ya waziri huyo inaendana na tamko la Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan lililotolewa Jumapili, lililolaani shambulio hilo na kulieleza kuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu pamoja na kuingilia mamlaka ya Saudi Arabia.
Wizara hiyo pia imesisitiza kuunga mkono haki ya Saudi Arabia kuchukua hatua halali za kulinda ardhi yake, raia wake na wakazi wake dhidi ya mashambulizi.