×

Rais Samia Aagiza Wakulima Wadogo Wanufaike na Shamba la Serikali Mbarali, Mbeya

RUJEWA, Mbeya — Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameonya dhidi ya watu wanaoweza kutumia nguvu zao za kiuchumi au nafasi zao kujinufaisha kupitia mpango wa Serikali wa shamba la Highland Estate lililopo wilayani Mbarali, mkoani Mbeya, badala ya kuwawezesha wakulima wadogo waliokusudiwa kunufaika.

Ndejembi amesema fedha zinazotolewa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kulirejesha shamba hilo chini ya usimamizi wa Serikali zinapaswa kuwanufaisha wakulima halisi, na si kuwa fursa kwa watu wachache wenye uwezo wa kifedha kujipatia manufaa binafsi.

Akizungumza wakati wa ziara yake Rujewa mkoani Mbeya, ambako aliwasilisha salamu za Rais Samia, Makamu wa Rais amesema Serikali tayari imetoa Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya malipo ya shamba hilo lenye takribani ekari 6,000, ambalo limefanyiwa uthamini wa Shilingi bilioni 30.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wakulima wadogo wanapata fursa ya kukodi maeneo ya shamba hilo kwa gharama nafuu, tofauti na gharama za kati ya Shilingi 600,000 na 700,000 kwa ekari zinazotozwa katika baadhi ya maeneo mengine.

Aagiza wakulima halisi kubainishwa

Katika kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa haki, Ndejembi amemwelekeza Waziri wa Kilimo kushirikiana na viongozi wa mkoa na wilaya, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi za Serikali kubaini wakulima halisi wanaostahili kunufaika na shamba hilo.

Amesisitiza kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kuingilia au kuhujumu mchakato huo kwa maslahi binafsi.

Makamu wa Rais pia ameonya dhidi ya watu wanaoweza kukodi mashamba hayo kutoka Serikalini kwa gharama nafuu na baadaye kuwakodishia wakulima wadogo kwa bei kubwa, hali inayoweza kuwanyima walengwa manufaa yaliyokusudiwa.

Amesema hakuna sababu ya kuwaonea huruma watu wanaotumia nafasi zao kujinufaisha wakati wakulima wa kawaida wakiendelea kukabiliwa na changamoto za upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Waziri wa Kilimo apewa maelekezo ya kuharakisha utekelezaji

Aidha, Ndejembi amemtaka Waziri wa Kilimo kuweka ukomo wa muda wa kukamilisha mchakato wa kuwapatia wakulima fursa ya kutumia maeneo hayo, akieleza kuwa wananchi wana mahitaji ya kila siku, yakiwemo kuhudumia familia na kusomesha watoto wao.

Akijibu maelekezo hayo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya malipo ya shamba hilo na inatarajia kukamilisha awamu mbili zilizobaki ndani ya miezi miwili.

Chongolo amehakikisha kuwa Serikali itaweka utaratibu utakaolinda maslahi ya wakulima wadogo na kuhakikisha wanapata fursa ya kunufaika na ardhi hiyo kwa gharama nafuu.

Amefafanua kuwa shamba hilo halitagawiwa kwa wananchi kama umiliki wa moja kwa moja, bali litaendeshwa kwa mfumo wa ukodishaji wa msimu chini ya usimamizi wa Serikali.

Serikali kusimamia haki za wakulima

Ndejembi amesisitiza kuwa kasi ya utekelezaji wa mpango huo lazima iendane na uadilifu na uwazi ili kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kuwasaidia wakulima waliopoteza maeneo yao kufuatia mabadiliko ya mipaka ya hifadhi inafikiwa.

Amesema ni muhimu kuhakikisha fursa hiyo inawafikia walengwa halisi badala ya kutekwa na watu wenye maslahi binafsi.

Hatua hiyo inalenga kuweka mazingira bora kwa wakulima wadogo kuendelea na shughuli za uzalishaji, kuongeza kipato na kuimarisha maisha yao pamoja na familia zao.

Leave a Comment