
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameingia katika hatua ya mwisho ya kuwania Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo ya mwaka 2026, inayotolewa na Bunge la Ulaya kwa kutambua mchango wa kipekee katika kutetea haki za binadamu na uhuru wa msingi.
Lissu ni miongoni mwa wateule watatu waliochaguliwa na kamati za Bunge la Ulaya kutoka orodha ya awali ya wagombea sita, hatua inayomuweka kiongozi huyo wa upinzani kutoka Tanzania miongoni mwa wanaowania tuzo hiyo ya kimataifa.
Wagombea wengine waliofikia hatua hiyo ni Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) pamoja na maofisa wake, na dada mapacha wa Iran, Taraneh na Romina Rahimi, wanaotajwa katika harakati za kutetea haki za binadamu na kupinga ukandamizaji nchini humo.
Katika orodha ya awali ya mwaka huu, wagombea wengine walikuwa Rais wa El Salvador, Nayib Bukele; Daktari wa watoto na mkurugenzi wa hospitali ya Gaza, Hussam Abu Safiya; pamoja na Standing Together, harakati inayowakutanisha raia wa Kiyahudi na Waarabu wa Palestina nchini Israel.
Kwa mujibu wa taarifa kuhusu mchakato huo, Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, anatarajiwa kumtangaza mshindi Alhamisi, Oktoba 22, 2026, huku hafla ya kukabidhi tuzo hiyo ikipangwa kufanyika Desemba 16, mwaka huu, mjini Strasbourg, Ufaransa.
Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo hutolewa kila mwaka na Bunge la Ulaya kwa watu, makundi au taasisi zinazotoa mchango wa kipekee katika kulinda haki za binadamu, uhuru wa mawazo na demokrasia. Tuzo hiyo ina thamani ya Euro 50,000.