×

Mwigulu Akutana na Rais wa AGRA, Aweka Wazi Mikakati ya Tanzania Kuimarisha Kilimo

DES MOINES, MAREKANI — Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekutana na Rais wa Shirika la AGRA, Bi. Alice Ruhweza, na kueleza mikakati ya Serikali ya kuimarisha sekta ya kilimo pamoja na kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji wa mazao nchini.

Mazungumzo hayo yamefanyika Oktoba 21, 2026, jijini Des Moines, katika Jimbo la Iowa, Marekani, pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), unaowakutanisha wadau mbalimbali wa kilimo na usalama wa chakula duniani.

Dkt. Mwigulu anashiriki mkutano huo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo kwa kuimarisha mifumo ya umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu bora, utafiti wa kilimo na huduma za ugani ili kuongeza tija na uzalishaji.

Amesema hatua nyingine zinazochukuliwa ni kuboresha upatikanaji wa maghala ya kuhifadhi mazao pamoja na miundombinu ya kuchakata mazao, hatua zinazolenga kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa na kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo.

Aidha, Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika sekta ya kilimo kwa kuondoa vikwazo vinavyowakabili, hususan upatikanaji wa ardhi, mafunzo ya kitaalamu na mitaji ya kuendesha shughuli zao za kilimo.

Kwa mujibu wa maelezo yake, Serikali inaendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha vijana kupata ardhi kwa ajili ya kilimo, kupata mafunzo na kuunganishwa na taasisi za kifedha ili waweze kupata mikopo kwa ajili ya kununua mbegu bora, zana za kilimo na pembejeo nyingine muhimu.

Hatua hizo zinatarajiwa kuchangia kuongeza uzalishaji, kuimarisha ajira kwa vijana na kuifanya sekta ya kilimo kuwa chanzo muhimu cha fursa za kiuchumi nchini.

Mkutano wa Borlaug Dialogue ni jukwaa la kimataifa linalowakutanisha viongozi, wataalamu na wadau wa sekta ya kilimo kujadili masuala yanayohusu uzalishaji wa chakula, ubunifu wa kilimo na mikakati ya kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula duniani.

Leave a Comment