×

Nicki Minaj Atajwa Kuchukua Nafasi ya Msemaji wa Ikulu ya Marekani,


Rapa maarufu wa Marekani, Nicki Minaj, amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutajwa kuwa huenda akachukua nafasi ya Msemaji Mkuu wa Ikulu ya White House, kufuatia kuondoka kwa Katie Zacharia katika nafasi hiyo siku tano tu baada ya kuanza kazi katika utawala wa Rais Donald Trump.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna tangazo rasmi kutoka White House linalothibitisha kuwa Minaj ameteuliwa au anazingatiwa rasmi kwa nafasi hiyo, licha ya mjadala huo kuendelea kuvuta hisia za mashabiki na wadau wa siasa nchini Marekani.

Mjadala huo ulianza kushika kasi baada ya Mkurugenzi wa Mawasiliano wa White House, Steven Cheung, kuchapisha video inayomuonyesha Minaj akiwa ndani ya ndege ya rais, Air Force One, akieleza mtazamo wake kuhusu utendaji wa uchumi wa Marekani chini ya uongozi wa Trump.

Cheung aliambatanisha video hiyo na ujumbe wa utani kwenye mtandao wa X, akidokeza kuwa huenda utawala wa Trump umempata msemaji mpya wa Ikulu.

Akaunti rasmi ya White House nayo ilijibu chapisho hilo kwa kutumia alama za macho, huku mshauri wa Trump, Alex Bruesewitz, akiwashirikisha mashabiki wa Minaj, maarufu kama Barbz, kwa kuwauliza maoni yao kuhusu uwezekano wa rapa huyo kupewa nafasi hiyo.

Minaj naye alijibu kwa kuchapisha bendera ya Marekani ikiambatana na emoji ya uso unaoonyesha wasiwasi, lakini hakutoa tamko la moja kwa moja kuthibitisha iwapo angependa kujiunga na utawala wa Trump katika nafasi hiyo.

Kuondoka kwa Katie Zacharia kwaibua mjadala
Jina la Minaj limeibuka katika kipindi ambacho nafasi ya msemaji wa White House iko wazi kufuatia kuondoka kwa Zacharia siku tano tu baada ya kuanza majukumu yake.

Zacharia alikabiliwa na ukosoaji kuhusu mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari, ambao ulidumu kwa muda mfupi na kutoa nafasi ya maswali kwa waandishi kutoka vyombo vitatu pekee.

Pia, sifa zake za kitaaluma ziliibua mjadala baada ya kukiri kuwa hakufaulu mtihani wa uwakili wa California. Baadaye aliondoka katika nafasi hiyo, hatua iliyozua maswali kuhusu nani angechukua jukumu la kuwasilisha misimamo ya utawala wa Trump kwa umma.


Nicki Minaj amekuwa akionyesha wazi kumuunga mkono Trump, akimsifu kuhusu uelewa wake wa uchumi, sera za kimataifa na namna anavyotekeleza majukumu yake.

Oktoba 25, 2026, Minaj alisafiri pamoja na Trump ndani ya ndege ya Air Force One kuelekea Michigan, ambako rais huyo alishiriki mkutano wa kampeni za kuwaunga mkono wagombea wa Republican kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula unaotarajiwa kufanyika Novemba 3, 2026.

Katika mkutano huo, Minaj alitoa ujumbe wa kumuunga mkono Trump na kuwataka wapiga kura kuwaunga mkono wagombea wa Republican, akieleza kuwa anaamini uongozi wa rais huyo umeleta matumaini mapya kwa Wamarekani.

Ushiriki wake katika shughuli hizo za kisiasa umeongeza mjadala kuhusu nafasi ya watu mashuhuri katika siasa za Marekani na namna umaarufu wao unavyoweza kutumika katika mawasiliano ya kisiasa.

Kwa sasa, White House haijamtangaza mtu atakayechukua nafasi iliyoachwa wazi na Zacharia. Hivyo, uwezekano wa Nicki Minaj kuwa Msemaji Mkuu wa Ikulu bado ni mjadala unaoendelea mitandaoni, bila uthibitisho wa uteuzi rasmi.

Endapo Minaj angepewa nafasi hiyo, angehusika katika kuwasilisha misimamo na sera za utawala wa Trump kwa umma pamoja na kujibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu shughuli za serikali.

Leave a Comment