
Kocha wa muda wa Yanga, Simon Dladla, leo Oktoba 26, 206 amekiri kuwa timu hiyo ina deni kubwa kwa mashabiki wake kufuatia matokeo yasiyoridhisha katika mchezo uliopita, akiahidi kufanya kazi kwa bidii ili kurejesha furaha kwa Wananchi.
Dladla amesema Yanga inahitaji kuwa makini zaidi katika kutumia nafasi za kufunga mabao, hasa inapocheza nyumbani, akisisitiza kuwa wachezaji wanapaswa kuwa wakali na kufanya maamuzi ya haraka na sahihi mbele ya lango la wapinzani.
“Tunacheza nyumbani, hivyo ni lazima tuwe wakali na wenye maamuzi haraka na sahihi mbele ya lango. Tunapaswa kutumia vizuri nafasi zetu na kuhakikisha tunapata matokeo tunayoyahitaji. Sisi ni wataalamu wa mchezo huu na tunaelewa changamoto zinazotukabili. Ninaamini tuko tayari,” amesema Dladla.
Kocha huyo ameeleza kuwa jukumu kubwa la kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri lipo mikononi mwa wachezaji, huku akibainisha kuwa mabadiliko ya kimfumo na kimbinu yatategemea wachezaji watakaokuwepo kwa ajili ya mchezo unaofuata.
Amesema benchi la ufundi linaendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza, likiwa na lengo la kuifanya Yanga icheze soka la kuvutia na kurejea katika ushindani unaoendana na matarajio ya klabu hiyo.
“Malengo makubwa ya Yanga ni kuhakikisha tunakuwa namba moja,” amesema Dladla.
Akizungumzia matokeo ya mchezo uliopita, Dladla amekiri kuwa kikosi hicho kiliwaangusha mashabiki wake kwa kushindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa, lakini amewataka Wananchi kuendelea kuwa na imani na timu yao.
Amesema wachezaji na benchi la ufundi wanafahamu matarajio ya mashabiki, hivyo wanapaswa kuonyesha mwitikio ndani ya uwanja kwa kupata matokeo mazuri, kufunga mabao na kuonyesha kiwango cha juu cha ushindani.
“Kwa Wananchi, tunafahamu kuwa tuliwakatisha tamaa katika mchezo uliopita kwa sababu hatukupata matokeo tuliyokuwa tunayatarajia. Tumeyatambua mapungufu yetu na tutafanya kazi kwa bidii. Tunafahamu kuwa tuna deni kubwa kwenu. Tunadaiwa magoli, tunadaiwa soka zuri na kiwango cha juu cha ushindani kila tunaposhuka uwanjani,” amesema Dladla.
Aidha, kocha huyo amewaomba mashabiki wa Yanga kuipa benchi la ufundi na wachezaji muda wa kufanya kazi, huku akiwataka kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuendelea kukipa nguvu kikosi hicho.
Amesisitiza kuwa timu itapambana kuhakikisha inapata matokeo yatakayorejesha tabasamu kwa mashabiki wake na kuwapa sababu ya kuendelea kuiamini klabu yao.