×

Video: Mwigulu Aagiza Hatua Kali Kwa Wanaochukua Sheria Mkononi

Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekemea vikali vitendo vya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi, huku akiviagiza vyombo vya dola kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 26, 2026, jijini Dodoma wakati akizungumza na wabunge wa Mkoa wa Ruvuma, kufuatia vurugu zilizotokea hivi karibuni kati ya wakulima na wafugaji, ambazo zimesababisha madhara mbalimbali yakiwemo vifo.

Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya uvunjifu wa sheria na kuwataka wananchi kutatua tofauti zao kwa kufuata taratibu zilizowekwa badala ya kutumia nguvu au kujichukulia hatua dhidi ya wenzao.

Amesema kujichukulia sheria mkononi ni kinyume cha Katiba na sheria za nchi, hivyo kila mwananchi anapaswa kuheshimu sheria na kuviachia vyombo vya dola kutekeleza majukumu yake.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha kuwa uuzaji na ugawaji wa maeneo unazingatia mipango na miongozo ya matumizi bora ya ardhi ili kuzuia migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Dkt. Mwigulu amesema matumizi ya ardhi yanapaswa kusimamiwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha makundi mbalimbali yanaendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa amani na usalama.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha ardhi inatumika kwa mujibu wa mipango iliyopo, akisisitiza kuwa usimamizi mzuri wa ardhi ni muhimu katika kuzuia migogoro na kulinda maisha ya wananchi.

Waziri Mkuu pia ametoa pole kwa wananchi wa Wilaya ya Tunduru na Watanzania wote walioathiriwa na matukio hayo, huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuhakikisha wote watakaobainika kuhusika na makosa wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha, amewataka wananchi kuendeleza utamaduni wa kuheshimiana, kuvumiliana na kushirikiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika shughuli zao za kila siku.

Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa amani na mshikamano ni tunu muhimu za Taifa ambazo zinapaswa kulindwa na kila Mtanzania, akibainisha kuwa tofauti zinazohusu shughuli za kiuchumi na matumizi ya ardhi zinapaswa kutatuliwa kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.

Amesema ushirikiano kati ya wananchi, viongozi wa maeneo na vyombo vya dola ni muhimu katika kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa njia za kisheria na kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.

Leave a Comment