
Vijana 114 wanaoishi katika mazingira magumu ya kimaisha wamekabidhiwa leseni za udereva bure Mkoani Arusha baada ya kuhitimu mafunzo ya udereva yalyoratibiwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani humo.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo leo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoani humo, ACP Zauda Mohamed amesema mafunzo hayo yalianza na vijana 126, ambapo kati ya 114 wamefanikiwa kuhitimu baada ya kufaulu mitihani na kupewa leseni rasmi za udereva.

ACP Zauda amesema utoaji wa mafunzo na leseni hizo za udereva kwa vijana hao wanaoishia katika mazingira magumu, unalenga kuwajengea vijana uwezo wa kutumia ujuzi walioupata kufungua fursa za kiuchumi kwa kujitafutia kipato ili kuboresha maisha yao.
Aidha, amewataka wahitimu hao kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani na kuwa mabalozi wema kwa watumiaji wengine wa barabara, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia wenye uhitaji katika jamii ili kuwainua kiuchumi.

Kwa upande wake mhitimu wa mafunzo hayo Bi. Emilia Frank, ameishukuru programu hiyo iliyoendeshwa kwa msaada kikosi cha usalama barabarani, akisema kupata leseni ya udereva ni hatua muhimu inayomfungulia fursa mpya za kujipatia kipato na kuboresha maisha yake.
Amesema atatumia fursa hiyo kwa uwajibikaji na kuzingatia sheria za usalama barabarani, huku akimshukuru mlezi wa programu hiyo kwa kuwaunga mkono hadi kufikia hatua ya kuhitimu na kukabidhiwa leseni zao.
