
Jina la Mini LED kwenye boksi la televisheni linaweza kumvutia mnunuzi anayetarajia kupata picha zenye ubora wa juu. Hata hivyo, wataalamu wa teknolojia wanaeleza kuwa jina hilo pekee halitoshi kubaini uwezo halisi wa televisheni, kwani ubora wa picha hutegemea pia mifumo inayotumika kudhibiti mwanga.
Teknolojia ya Mini LED hutumia taa ndogo zinazowekwa nyuma ya paneli ya televisheni, hivyo kuruhusu matumizi ya taa nyingi zaidi na udhibiti wa mwanga katika maeneo mbalimbali ya skrini.
Mfumo huo unapotekelezwa vizuri, unaweza kuboresha ubora wa picha kwa kufanya maeneo meusi yaonekane meusi zaidi, huku sehemu zenye mwanga zikibaki angavu na zenye undani. Hali hiyo husaidia kuboresha utofauti wa mwanga na giza katika picha, unaojulikana kama contrast.

1. ANGALIA MFUMO WA LOCAL DIMMING
Moja ya mambo muhimu kwa mnunuzi ni kuchunguza kama televisheni ina mfumo wa hardware local dimming, unaowezesha mwanga kupunguzwa au kuongezwa katika maeneo tofauti ya skrini.
Mfumo huo hudhibiti mwanga wa taa zilizopo nyuma ya paneli kulingana na sehemu za picha zinazoonyeshwa. Kwa mfano, wakati skrini inaonesha eneo lenye giza karibu na sehemu yenye mwanga mkali, mfumo unaweza kupunguza mwanga katika eneo la giza na kuongeza mwanga katika eneo linalohitaji kung’aa zaidi.
Udhibiti huo unaweza kusaidia kuboresha utofauti wa picha na kufanya maudhui yenye maeneo ya mwanga na giza yaonekane kwa undani zaidi.

2. IDADI YA DIMMING ZONES NI MUHIMU
Jambo jingine la kuzingatia ni idadi ya dimming zones, yaani maeneo ya taa yanayoweza kudhibitiwa kwa kujitegemea.
Kwa ujumla, televisheni yenye maeneo mengi ya udhibiti wa mwanga inaweza kuwa na uwezo wa kudhibiti mwanga kwa usahihi zaidi kuliko ile yenye maeneo machache, iwapo mifumo mingine inalingana.
Hata hivyo, idadi kubwa ya maeneo hayo haimaanishi moja kwa moja kuwa televisheni hiyo ina picha bora zaidi. Ubora pia hutegemea jinsi mfumo wa udhibiti wa mwanga unavyofanya kazi, ubora wa paneli na uwezo wa kuchakata picha.
Kwa hiyo, mnunuzi anashauriwa kulinganisha vipengele hivyo badala ya kuamua kwa kuangalia idadi ya maeneo ya mwanga pekee.
3. FAHAMU MFUMO WA FULL ARRAY LOCAL DIMMING
Mfumo wa Full Array Local Dimming (FALD) ni teknolojia inayoweka taa nyuma ya paneli ya televisheni na kuziruhusu kudhibitiwa katika maeneo mbalimbali ya skrini.
Mpangilio huo husaidia mfumo kurekebisha mwanga kulingana na maudhui yanayooneshwa, badala ya kutegemea mwanga unaosambazwa kwa namna ileile katika skrini nzima.
Kwa televisheni za Mini LED, mpangilio na udhibiti wa taa ni miongoni mwa vipengele vinavyoweza kuathiri utendaji wa picha. Kampuni ya TCL imeeleza umuhimu wa kuzingatia mifumo hiyo wakati wa kulinganisha televisheni za teknolojia hiyo kutoka kwa wazalishaji mbalimbali.
MNUNUZI ANAPASWA KUZINGATIA NINI?
Kabla ya kununua televisheni yenye teknolojia ya Mini LED, ni muhimu kuchunguza vipengele vyake vya kiufundi badala ya kutegemea jina lililoandikwa kwenye boksi.
Mnunuzi anapaswa kuuliza kama televisheni ina mfumo wa local dimming, ina dimming zones ngapi na taa zimepangwa kwa mfumo gani nyuma ya paneli.
Pia, ni vyema kulinganisha ubora wa picha katika mazingira halisi ya matumizi, kwa kuangalia namna televisheni inavyoonesha maeneo meusi, sehemu zenye mwanga mkali na undani wa picha.
Kwa kufanya hivyo, mnunuzi anaweza kuwa na nafasi nzuri ya kuchagua televisheni inayokidhi mahitaji yake, badala ya kuamua kwa kutegemea jina la Mini LED pekee.