×

Hofu Yatanda Hormuz Baada ya Meli za Mafuta Kushika Moto

Jeshi la Iran limedai kuwa angalau meli nne za mafuta zimekumbwa na moto baada ya kugonga migodi ya baharini wakati zikijaribu kupita katika Mlango-Bwawa wa Hormuz, madai yaliyotolewa siku moja baada ya jeshi la Marekani kusema kuwa limesafisha njia muhimu za usafiri katika eneo hilo.

Katika taarifa yake, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) limesema meli tatu za mafuta zililipuka na kushika moto ndani ya saa 24 baada ya kugonga migodi zilipokuwa zikijaribu kutumia njia ya kusini ambayo Iran imeitaja kuwa hairuhusiwi.

Taarifa hiyo imesema meli hizo zilizima mifumo yake ya rada na urambazaji, huku zikipuuza maonyo yaliyotolewa na jeshi la wanamaji la IRGC. Hata hivyo, haikufahamika mara moja ni lini matukio hayo yalitokea wala meli hizo zilikuwa na bendera za nchi gani.

Baadaye siku hiyo, jeshi la Iran liliripoti kuwa meli nyingine ya mafuta ilipata madhara na kushika moto upande wa mashariki wa Mlango-Bwawa wa Hormuz baada ya kugonga migodi ya baharini katika eneo lililotangazwa kuwa na vikwazo na hatari.

Katika wiki za hivi karibuni, Iran imeripoti matukio kadhaa ya meli kugonga migodi ya baharini, huku Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ikisisitiza kuwa migodi yote katika njia kuu za usafiri wa majini imeondolewa.

Hata hivyo, msemaji wa IRGC, Hossein Mohebi, amepinga madai hayo na kuitaka Marekani kutoa ushahidi huru kuthibitisha kuwa imefanikiwa kuondoa migodi katika Mlango-Bwawa huo, badala ya kutoa matamko pekee.

Tangu kuanza kwa vita Februari 28, Iran imeweka vikwazo vikali kwa usafiri wa meli katika Mlango-Bwawa wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha takribani moja ya tano ya matumizi ya mafuta na gesi duniani.

Kwa upande wake, Marekani imeweka zuio dhidi ya bandari za Iran na kusaidia meli za mafuta kupita katika njia hiyo ya kimkakati. Siku ya Jumapili, CENTCOM ilisema imesaidia nchi za Ghuba kusafirisha mapipa bilioni 1.5 ya mafuta kupitia Hormuz tangu kipindi cha kiangazi.

Iran inachukulia meli zinazotumia njia ya kusini karibu na pwani ya Oman kuwa zinatumia njia isiyoruhusiwa. Katika taarifa yake, IRGC imesema wamiliki wa meli na wafanyakazi wake wanapaswa kuwajibika wanapoamua kutumia njia hiyo, huku ikipinga madai ya Marekani kuhusu usalama wa njia kuu za usafiri.

Wakati huohuo, shirika la Uingereza linalofuatilia usalama wa biashara ya majini, UKMTO, limeripoti kuwa chombo cha majini kilishika moto na kuzama takribani maili tisa za baharini kaskazini mwa Khasab, nchini Oman.

Kwa mujibu wa UKMTO, mamlaka za eneo hilo zilitambua chombo hicho kuwa ni jahazi, huku wafanyakazi wake wote wakihamishwa salama kabla ya kuzama kwa chombo hicho.

Katika tukio jingine, IRGC imedai kuwa kitengo chake cha vita vya kielektroniki kilifanikiwa kukamata ndege isiyo na rubani ya Marekani aina ya MQM-170 wakati wa operesheni iliyofanyika upande wa magharibi wa Mlango-Bwawa wa Hormuz.

Hata hivyo, madai ya Iran kuhusu meli zilizogonga migodi na kukamatwa kwa ndege hiyo isiyo na rubani hayakuwa yamethibitishwa kwa kujitegemea katika taarifa hiyo.

Leave a Comment