×

BOT Yasaini Hati Tatu za Makubaliano, Kuibua Nguvu Mpya ya Elimu

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesaini hati tatu za makubaliano ya ushirikiano na taasisi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha elimu ya fedha, kuongeza uelewa wa masuala ya kiuchumi na kuwajengea wananchi uwezo wa kusimamia rasilimali zao kwa ufanisi.

Hati hizo zimesainiwa Oktoba 29, 2026, kupitia Chuo cha Benki Kuu jijini Mwanza, zikihusisha Benki Kuu ya Madagascar, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Chama cha Wafanyakazi Wakusanya Mapato Tanzania (TAREWU).

Hafla ya utiaji saini ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi hizo, akiwemo Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, Gavana wa Benki Kuu ya Madagascar, Aivo Handriatiana Andrianarivelo, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, Katibu Mkuu wa TAREWU, Michael Marere, pamoja na Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu, Tawi la Mwanza, Dkt. Nicas Yabu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Gavana Tutuba amesema elimu ya fedha ni nyenzo muhimu inayowawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya fedha, kuweka akiba na kufanya uwekezaji wenye tija.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo unalenga kuwapatia wananchi maarifa na ujuzi utakaowasaidia kutumia rasilimali walizonazo katika shughuli za kiuchumi, kuongeza uzalishaji na kuchangia upatikanaji wa ajira.

Kwa upande wake, Profesa Anangisye ameeleza utayari wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuendelea kushirikiana na BoT katika kuendeleza elimu ya usimamizi wa fedha.

Amesema UDSM ina wataalamu wenye ujuzi na uzoefu katika masuala ya uchumi ambao wanaweza kutoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa makubaliano hayo na kufanikisha malengo yaliyowekwa.

Kupitia ushirikiano huo, BoT inalenga kupanua wigo wa elimu ya fedha kwa wananchi, kuwajengea uwezo wa kutumia huduma na fursa za kifedha kwa usahihi, pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa wa masuala ya kifedha nchini ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Leave a Comment