×

Kaka wa Lissu, Wakili Alute Mughwai Lissu Afariki Dunia

Wakili Alute Mughwai Lissu, ambaye ni kaka wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amefariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 1, 2026, katika Hospitali ya Serian jijini Arusha.

Taarifa za kifo cha Wakili Alute zimethibitishwa na ndugu wa karibu wa familia amezungumza na mtangazaji wa Global TV Online, Victor Korumba Moshi, maarufu kama Mwandishi Msomi.

Akizungumzia mazingira ya kifo hicho, ndugu huyo amesema kwa sasa familia haipo tayari kutoa maelezo zaidi, akibainisha kuwa marehemu alikuwa akiugua kwa muda mrefu.

Aidha, amethibitisha kuwa msiba upo jijini Arusha, huku baadhi ya wanafamilia wakielekea eneo hilo kwa ajili ya kushiriki katika shughuli za msiba.

Katika maelezo yake, amesema:

“Ni taarifa za kweli, msiba upo Arusha na mimi naelekea huko.”

Hadi sasa, familia haijatoa taarifa rasmi zaidi kuhusu ugonjwa uliokuwa ukimsumbua marehemu wala mipango ya mazishi.

Ndugu, jamaa na marafiki wanaendelea kuungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki cha majonzi.

Stori na Victor Korumba Moshi, Mwandishi Msomi | Global TV Arusha

Leave a Comment