×

Marekani Kuiondoa Rwanda na Afrika Kusini Kwenye Mpango wa AGOA

 

Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, umetangaza mpango wa kuiondoa Rwanda na Afrika Kusini katika mpango wa upendeleo wa kibiashara wa Marekani unaojulikana kama AGOA, kuanzia Januari Mosi mwaka 2027.

Uamuzi huo unatarajiwa kuathiri biashara kati ya nchi hizo na Marekani, kupitia mpango wa African Growth and Opportunity Act (AGOA), unaozipa nchi za Afrika zinazokidhi masharti fursa ya kuuza maelfu ya bidhaa katika soko la Marekani bila kutozwa ushuru wa forodha.

Mwakilishi wa Biashara wa Marekani, Jamieson Greer, amesema tathmini ya kila mwaka ya mpango huo imebaini kuwa Rwanda na Afrika Kusini zinakiuka baadhi ya masharti yanayohitajika ili kuendelea kunufaika na fursa hiyo.

Kwa mujibu wa Greer, serikali ya Marekani tayari imezifikishia nchi hizo taarifa kuhusu uamuzi huo, ikieleza kuwa kuna masuala yanayohusiana na vikwazo vya biashara na uwekezaji wa Marekani, usalama wa taifa pamoja na maslahi ya sera za kigeni.

Kwa upande wa Rwanda, Marekani imeeleza pia wasiwasi kuhusu masuala ya haki za binadamu, uhuru wa kisiasa, utawala wa sheria na haki za wafanyakazi.

Hatua hiyo inakuja wakati ambapo uhusiano kati ya Washington na Kigali ukiwa katika mvutano, kufuatia vikwazo vilivyowekwa na Wizara ya Fedha ya Marekani dhidi ya Wizara ya Ulinzi ya Rwanda.

Taarifa ya Reuters pia inaeleza kuwa Afrika Kusini iliingiza bidhaa zenye thamani ya takribani dola bilioni 1.7 za Marekani kupitia AGOA mwaka 2025, zikiwemo vipuri vya magari, matunda jamii ya machungwa na mvinyo.

Rwanda nayo inanufaika kupitia mauzo ya kahawa na madini.Hatua hiyo inaweza kuongeza gharama za bidhaa zitakazoingia katika soko la Marekani kutoka nchi hizo, endapo zitaanza kutozwa ushuru wa kawaida badala ya kunufaika na upendeleo wa AGOA.

Hata hivyo, Marekani imesema nchi hizo zinaweza kuchukua hatua zinazohitajika ili kukidhi vigezo vya mpango huo na kurejesha hadhi yake.

Leave a Comment