×

Mshambuliaji wa Tenerife Jesus de Miguel Afariki Baada Ya Kugongana na Kipa Uwanjani

Mshambuliaji wa klabu ya CD Tenerife ya Hispania, Jesus de Miguel Alameda, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 30 baada ya kupata majeraha makubwa ya kichwa na kifua kufuatia kugongana na mlinda mlango wa FC Andorra, Jesus Owono, katika mchezo wa ligi daraja la pili nchini humo.

Tukio hilo lilitokea Jumatatu Novemba  wakati timu hizo zikicheza mchezo uliokuwa ukielekea ukingoni kwa matokeo ya sare ya mabao 2-2, ambapo dakika saba za nyongeza zilikuwa zimeongezwa.

Kwa mujibu wa taarifa za mchezo huo, Owono alikimbia kuelekea katikati ya uwanja kwa lengo la kuondoa mpira mrefu, lakini goti lake liligongana na mwili wa De Miguel, ambaye alianguka na kubaki bila kusogea uwanjani.

Madaktari waliokuwa uwanjani walitoa huduma ya kwanza kabla ya mshambuliaji huyo kukimbizwa hospitalini kwa gari la wagonjwa kutoka Uwanja wa Estadio Heliodoro Rodriguez Lopez.

Hali yake ilielezwa kuwa mbaya Jumatatu, hata hivyo ilizidi kuwa mbaya Jumanne asubuhi na hatimaye kufariki dunia saa 10:00 alfajiri kwa saa za Hispania.

Klabu ya Tenerife imethibitisha kifo hicho kupitia taarifa iliyosema imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mchezaji huyo, huku ikitoa pole kwa familia, ndugu, marafiki na mashabiki wa klabu hiyo.

Katika tukio hilo, mwamuzi wa mchezo alimpatia kipa Owono kadi nyekundu ya moja kwa moja kabla ya kusitisha mchezo kutokana na uzito wa tukio hilo.

Kifo cha De Miguel kimeibua majonzi makubwa katika ulimwengu wa soka, huku klabu ya FC Andorra, ambayo ilikuwa mpinzani wa Tenerife katika mchezo huo, nayo ikitoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na klabu yake.

Aliyekuwa beki wa Barcelona na mmiliki mwenza wa FC Andorra, Gerard Pique, pamoja na Rais wa La Liga, Javier Tebas, ni miongoni mwa viongozi wa soka walioeleza masikitiko yao.

Nyota wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe, pia alitoa salamu za rambirambi kupitia mitandao ya kijamii.

Kufuatia kifo hicho, Shirikisho la Soka la Hispania limetangaza kuahirishwa kwa michezo ya Kombe la Hispania iliyokuwa imepangwa kuchezwa Jumanne, ikiwa ni pamoja na michezo ya Copa del Rey na Copa de la Reina.

Leave a Comment