
WASHINGTON, Marekani – Rais wa Marekani, Donald Trump, amekiri kuwa vita dhidi ya Iran vilichangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kwa chama chake cha Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula (Midterm Elections), baada ya chama cha Democratic kupata ushindi na kudhibiti Bunge la Marekani.
Trump amekiri hayo Jumatano, Novemba 5, 2026, akijibu swali kuhusu kauli ya Makamu wa Rais JD Vance, aliyesema vita vya Iran ndiyo sababu kuu iliyosababisha Republican kupoteza uchaguzi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la ujenzi wa ukumbi mpya wa White House, Trump alisema anakubaliana kwa kiasi kikubwa na tathmini hiyo, akieleza kuwa vita hivyo vilichangia kupanda kwa bei ya petroli kwa muda mfupi.

“Hilo kwa kiasi kikubwa ni kweli kwa sababu vilipandisha bei ya petroli kidogo kwa muda mfupi,” alisema Trump.
Hata hivyo, rais huyo alisisitiza kuwa bado anaamini uamuzi wa kuishambulia Iran ulikuwa sahihi na kwamba angechukua hatua hiyo tena kama angepewa nafasi nyingine.
Alidai kuwa hatua hiyo ilikuwa muhimu kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia.
Katika hatua nyingine, Trump alimtetea Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, akisema anafanya kazi nzuri na kwamba hana mpango wa kumwondoa katika nafasi hiyo.
Awali, Vance alisema Republican wanapaswa kukubali ukweli kwamba vita vya Iran vimewaathiri kisiasa, akibainisha kuwa baadhi ya wapiga kura waliowaunga mkono Trump na Vance mwaka 2024 walihamia upande wa Democratic katika uchaguzi wa 2026.
Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Vance alisema vita hivyo, pamoja na hali ya uchumi, vilikuwa miongoni mwa sababu zilizowafanya wapiga kura kuachana na Republican.
Alisisitiza kuwa mjadala wowote kuhusu mustakabali wa chama hicho unapaswa kuanzia katika kukubali sababu za kushindwa kwao.
Kauli za Vance zimekuja wakati kukiwa na mjadala kuhusu nafasi yake ndani ya Republican kuelekea uchaguzi wa urais wa mwaka 2028, ingawa bado hajatangaza rasmi nia ya kugombea urais.
Wakati huohuo, Kiongozi wa Democratic katika Seneti, Chuck Schumer, ameitaka serikali ya Trump kumaliza vita dhidi ya Iran, akionya kuwa chama chake kinaweza kutumia mamlaka ya Bunge kuhusu fedha za serikali kushinikiza kusitishwa kwa vita hivyo.
Schumer alisema Marekani haiwezi kuendelea na vita bila kuzingatia ridhaa ya wananchi.
Katika uchaguzi huo, Democratic ilifanikiwa kupata udhibiti wa Baraza la Wawakilishi na Seneti, hatua inayowapa uwezo mkubwa wa kushawishi miswada ya sheria, kufanya uchunguzi kuhusu utendaji wa serikali ya Trump na kuzuia baadhi ya uteuzi wa rais.
Matokeo hayo yamehusishwa na kutoridhika kwa wananchi kuhusu gharama za maisha, ushuru wa bidhaa kutoka nje na athari za vita vya Iran katika uchumi wa Marekani.
Pamoja na kushindwa kwa chama chake, Trump amedokeza kuwa bado anaweza kutumia mamlaka yake ya kura ya turufu (veto) kupinga miswada ambayo haitakubaliana na sera zake.
Kwa upande mwingine, White House imeendelea kuonyesha kuwa Trump bado ana mamlaka ya kuiongoza Marekani, kupitia ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wa X uliosomeka: “Trump bado ni Rais wenu.”
Ushindi wa Democratic umefungua ukurasa mpya wa mvutano wa kisiasa nchini Marekani, huku vita vya Iran, uchumi na mwelekeo wa sera za nje vikiwa miongoni mwa masuala yanayotarajiwa kutawala mijadala ya kisiasa katika kipindi kijacho.