×

TFF Yatangaza Ratiba ya Uchaguzi Mkuu Simba, Kampeni Kuanza Januari 7, 2027

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetangaza rasmi ratiba ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Simba Sports Club utakaofanyika Januari 30, 2027, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa Novemba 6, 2026, uchaguzi huo utafanyika kwa kuzingatia Ibara ya 37 ya Katiba ya Simba Sports Club, toleo la 2018, pamoja na marekebisho yaliyopitishwa katika Baraza la Wanachama wa Simba lililofanyika Februari 18, 2026.

Mchakato wa uchaguzi utaanza Novemba 16 hadi 20, 2026, ambapo fomu za wagombea zitatolewa na kurejeshwa. Novemba 21 hadi 23, Kamati ya Uchaguzi itafanya uhakiki wa fomu za wagombea, huku Novemba 25 na 26 zikitengwa kwa ajili ya rufaa zinazohusu wagombea walioenguliwa.

Novemba 27, majina ya wagombea waliokidhi vigezo yatatangazwa na mapingamizi dhidi yao kupokelewa. Novemba 28 na 29, Kamati itapokea mapingamizi hayo, kabla ya kuyafanyia kazi na kuyasikiliza katika hatua zitakazofuata.

Desemba 4 na 5, 2026, zimepangwa kwa ajili ya usaili wa wagombea, huku Desemba 6 Kamati ikitoa maamuzi kuhusu mapingamizi. Desemba 7, majina ya wagombea waliokidhi vigezo yatatangazwa.

Katika hatua za rufaa, kuanzia Desemba 8 hadi 12, rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi zitawasilishwa katika Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF. Desemba 13 hadi 17, Kamati hiyo itasikiliza rufaa, kabla ya kutoa maamuzi Desemba 18.

Desemba 19, Sekretarieti itawasilisha kesi za maadili katika Kamati ya Maadili. Desemba 20 hadi 24, Kamati ya Maadili itasikiliza mashauri, huku Desemba 25 ikipangwa kuwa siku ya kutoa maamuzi.

Desemba 26 hadi 30, rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Maadili zitawasilishwa katika Kamati ya Rufaa. Desemba 31, 2026 hadi Januari 4, 2027, Kamati ya Rufaa itasikiliza rufaa hizo na Januari 5 kutoa maamuzi.

Januari 6, 2027, Kamati ya Uchaguzi itatangaza orodha ya mwisho ya wagombea waliokidhi vigezo, huku kampeni za uchaguzi zikitarajiwa kuanza Januari 7 hadi 29, 2027.

Uchaguzi Mkuu wa Simba SC unatarajiwa kufanyika Januari 30, 2027.

Katika tangazo hilo, TFF imeeleza kuwa nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti, nafasi moja, pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, nafasi tano.

Fomu za kugombea zitatolewa kuanzia Jumamosi, Novemba 16 hadi 20, 2026, katika Ofisi za TFF zilizopo Karume, Ilala, Dar es Salaam, na katika ofisi za Simba Sports Club.

Ada ya fomu kwa nafasi ya Mwenyekiti ni Shilingi 300,000, huku fomu ya nafasi ya Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ikiwa Shilingi 150,000.

Malipo yatafanyika kupitia akaunti ya Simba Sports Club katika Benki ya CRDB, namba 01J1026761801, kwa jina la akaunti Simba Sports Club, au kwa kutumia mfumo wa PAY IN SLIP.

Kwa mawasiliano zaidi, waombaji wametakiwa kupiga simu namba 0714 595452.

Tangazo hilo limesainiwa na Wakili Kiongozi Kibamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, tarehe 6 Novemba 2026.

Leave a Comment