
Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga maarufu kama Nandy ameonyesha mafanikio yake katika muziki baada ya kujizawadia nyumba mpya ya kifahari katika kipindi cha kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Nandy ameweka wazi mafanikio hayo kupitia ukurasa wake wa Instagram, Novemba 8, 2026, kwa kushirikisha picha na video za nyumba hiyo huku magari yake ya kifahari yakiwemo Mercedes-Benz G-Wagon na Nissan V8 yakionekana yakiwa yameegeshwa ndani ya eneo la makazi hayo.

Katika ujumbe wake, Nandy ameeleza kuwa amefanikisha ndoto yake ya kumiliki nyumba binafsi kupitia kibali na rehema za Mungu, akiwashukuru mashabiki, vyombo vya habari, kampuni na wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakimuunga mkono katika safari yake ya muziki.
“Nimeweza kujizawadia nyumba kwenye mwaka wangu wa kuzaliwa, si mimi peke yangu bila nyie mimi si kitu,” aliandika Nandy.
Aidha, ameupongeza uongozi wake kwa kusimama naye na kumpa nguvu ya kutimiza ndoto zake, huku akiahidi kuendelea kuwapa mashabiki wake muziki mzuri na kuwataka waendelee kumuunga mkono katika safari yake ya kisanaa.

MASHABIKI WAMPA PONGEZI
Baada ya kuweka wazi mafanikio hayo, mashabiki na wadau mbalimbali wamejitokeza katika sehemu ya maoni kumpongeza Nandy kwa hatua hiyo, huku wengi wakieleza kufurahishwa na namna ambavyo amekuwa akitimiza ndoto zake.
Baadhi ya mashabiki wamempongeza kwa kutimiza ndoto ya kumiliki nyumba binafsi, wengine wakitumia nafasi hiyo kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa na kumtakia mafanikio zaidi katika maisha na muziki wake.

Miongoni mwa maoni yaliyovutia ni shabiki mmoja aliyeandika, “Hatimaye ndoto yako umetimiza, wewe mwanamke ukipanga kitu lazima utimize,” huku mwingine akitania kuwa muziki una fedha.
Wengine wamehusisha mafanikio hayo na mijadala ya magari na nyumba za kifahari zinazozungumzwa kwenye mitandao ya kijamii, wakiyachukulia kama sehemu ya mafanikio ya wasanii wa Bongo Fleva.