
WASHINGTON, MAREKANI: Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuna matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano yatakayomaliza vita kati ya Marekani na Iran, akidai kuwa mapigano hayo kwa upande wa kijeshi yamefikia mwisho.Trump alitoa kauli hiyo Jumatatu, baada ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, katika Ikulu ya White House, ambapo walijadili hali ya Mashariki ya Kati na uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano kati ya Washington na Tehran.
Akizungumza na waandishi wa habari, Trump alisema anaamini kuwa vita dhidi ya Iran kwa upande wa kijeshi vimekwisha kwa kiasi kikubwa, huku akieleza kuwa Marekani inaendelea kudumisha hali iliyopo wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea.
Alidai kuwa uwezo wa Iran umeathirika kwa kiasi kikubwa, lakini akasisitiza kuwa bado kuna umuhimu wa kuhakikisha kunapatikana suluhisho la muda mrefu litakalodhibiti mpango wa nyuklia wa Iran.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema uwezekano wa Marekani kurejea kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran ni mdogo sana.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Marekani bado iko tayari kuchukua hatua za kijeshi iwapo itahitajika, akieleza kuwa washirika wake muhimu katika eneo la Ghuba wanapendelea hali ya sasa iendelee kudumishwa.
“Tunaona dalili nzuri za kuelekea kumalizika kwa mzozo huu, na tutahakikisha maslahi ya Marekani yanalindwa wakati wote,” alisema Trump.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, alisema mazungumzo yake na Trump pamoja na Makamu wa Rais JD Vance yalikuwa mazuri na yalijikita katika kutafuta njia za kuendeleza mazungumzo kati ya Marekani na Iran.
Kupitia mtandao wa X, kiongozi huyo alisema wamejadili hali ya eneo hilo na namna ya kuendeleza mazungumzo yatakayowezesha kufikiwa kwa makubaliano na kurejesha amani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kauli za viongozi hao zinaashiria kuendelea kwa juhudi za kidiplomasia za kutafuta suluhu ya mzozo huo, ingawa bado haijabainika ni lini makubaliano rasmi yanaweza kufikiwa au masharti yatakayowekwa kwa pande zinazohusika.
Miongoni mwa masuala muhimu yanayobaki kuwa kitovu cha mazungumzo ni mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran na namna ya kuhakikisha usalama na utulivu wa muda mrefu katika eneo la Ghuba.