The House of Favourite Newspapers

FPCT,ERIKS wahuisha sauti za watoto wenye ulemavu

0

Baadhi ya watoto wenye ulemavu wakiwa kwenye picha ya pamoja na aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dokta Asha-Rose Migiro pamoja na viongozi wa FPCT.Baadhi ya watoto wenye ulemavu wakiwa kwenye picha ya pamoja na aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dokta Asha-Rose Migiro pamoja na viongozi wa FPCT.
KASHINDYE ATHUMANI

Mmoja wa walemavu hao Kashinde Athumani akizungumza jambo.

Katika mikutano mbalimbali kati ya watoto wenye ulemavu na viongozi wa serikali wakiwemo wale wanaofanya maamuzi, zimekuwa zikielezwa changamoto mbalimbali ambapo imebainika Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) na ERIKS wamehuisha uwezo wa watoto hao kupaza sauti zao.

Watoto hao kabla ya FPCT kuanzisha mpango wa kuwasaidia, walijiona kama waliotengwa lakini sasa angalau wana uwezo wa kupaza sauti zao kwa jamii inayowazunguka wakieleza changamoto wanazopitia kama wanavyoeleza hapa chini;

”Kwanza, sisi watoto wenye ulemevu tumekuwa tukitengwa kwenye mambo mbalimbali kama vile elimu kutokana na kutokuwepo na walimu maalum, vifaa vya kufundishia na dhana mbaya juu yetu iliyokuwa imejengeka kwenye jamii.

”Wazazi wetu walikuwa wakituona sisi kama mzigo au tusio na thamani. Matokeo yake sasa tumekuwa tukikosa elimu na msaada kutoka kwa familia zetu na jamii inayotuzunguka, mazingira yanayotufanya tuishie kwenye kuwa ombaomba.

“Serikali na mashirika ya misaada katika kipindi cha nyuma walikuwa hawatusaidii kwa lolote, hawakutilia maanani mahitaji yetu, matokeo yake sasa tumekuwa tumetengwa kwenye masuala muhimu kama vile elimu na shughuli mbalimbali za kijamii.

“Hatukuwa na uwezo wa kutengeneza vipato, ndoto za kuingia kwenye maisha ya ndoa na kupata watoto hatukuwa nazo. Kimsingi tumekuwa kwenye wakati mgumu sana. Msaada tuliokuwa tunapata ulikuwa mdogo.

“Sasa ndiyo tunaona kuwa, kama ndugu zetu wangetupa nafasi za kupata elimu huenda maisha yetu ya baadaye yangekuwa yenye mwanga lakini tulitengwa na kuachwa kwenye umasikini,” wanaeleza watoto hao.

Hivyo watoto Baraza la Watoto Wenye Ulemavu wameitaja FPCT na washirika wake ambao ni ERIKS kama watu wa pekee ambao wamewafanya wajisikie kuwa nao ni binadamu kama wengine kwani wamekuwa wakiwasaidia katika kupata elimu juu ya haki zao za msingi na namna ya kukabiliana na changamoto wanazopitia. Wasikie watoto hao wanavyowapongeza FPCT na ERIKS.

“Sisi watoto wenye ulemavu sasa tunajiona tuko salama na tumepata ujasiri na uelewa juu ya haki zetu hasa baada ya FPCT na ERIKS kuandaa mpango wa kutusaidia. Wametuunganisha na watoto wenzetu wasio walemavu, kujifunza juu ya haki za watoto, kujadili haki zetu na changamoto tunazopitia, kuiamsha serikali na wadau wengine kutusaidia.

“Miradi mbalimbali iliyokuwa inaandaliwa na FPCT imewafanya wazazi na jamii kwa ujumla kuona umuhimu wetu kwenye jamii na kujua majukumu waliyonayo katika kuhakikisha tunaishi maisha salama.

“Na sasa tunaona mabadiliko makubwa kwani wazazi, wanajamii na walimu angalau wanajali haki zetu na wanatusaidia katika kukabiliana na changamoto tunazopitia.

Baraza la watoto wenye ulemavu mkoa wa Arusha kupitia mwenyekiti wake wameitaka serikali iweke bajeti kwa ajili ya watoto wenye ulemavu na si kuwaachia FPCT na ERIKS kama vile ndiyo watu pekee wenye jukumu hilo.

Mwenyekiti kutoka Mkoa wa Tabora alisema: “Tulishangaa kuona FPCT na ERIKS wanatuandalia mikutano na viongozi wa wilaya na mikoa kisha kujadili juu ya matatizo ya kielimu tunayokumbana nayo wakati hilo ni jukumu la serikali. Ila tunayo furaha kusikia serikali imeahidi kututatulia matatizo yetu.

Viongozi wa watoto wenye ulemavu mkoani Rukwa walisema kuwa, baraza lao linafanya kazi kubwa ya kuwashinikiza viongozi na wafanya maamuzi wengine kuyatilia maanani mahitaji yao ila tatizo ni kwamba baraza hilo halikutani mara kwa mara.

Hivyo jitihada zinahitaji kuhakikisha baraza lao linakutana mara kwa mara ili kuweza kupata nafasi ya kujadili matatizo yao na changamoto zao mara kwa mara bila kuwategemea tu FPCT na ERIKS.

Huko Shinyanga, mwenyekiti wa baraza la watoto anasema kuwa, kumekuwa na ongezeko la kuripotiwa kwa matukio ya watoto kufanyiwa vitendo vibaya, na hii ni kutokana na mchango mkubwa wa FPCT na ERIKS ambao waliandaa mradi mkoani mwao.Kwa hiyo sapoti bado inahitajika ili kuwezesha elimu itakayosaidia kuongeza uelewa wa watu juu ya haki za watoto inaenea.

Kauli za watoto wenye ulemavu kutoka kwenye mabaraza ya mikoa mbalimbali
Clara Damian (mwenye ulemevu wa macho) kutoka Arusha anasema:
Kupitia baraza hili nimejua haki zangu. Nimekuwa mshauri mzuri kwa watoto wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kuwataka wazazi kuwajali na kuwapeleka shule badala ya kuwafungia ndani.

Pia ninao ujasiri wa kuandaa mikutano na waandishi kisha kueleza mambo mbalimbali yanayotuhusu kupitia redio na televisheni. Pia naweza kukutana na viongozi wa serikali na kuwahimiza kuzilinda haki zetu na kutatua changamoto zinazotukabili.

Emmanuel Mpozi kutoka Mbeya: “Ninao ujasiri wa kusimama popote na kuzielezea haki zetu kwenye jamii, na hii yote ni kutokana na mchango mkubwa wa FPCT na ERIKS.
Imeandikwa na Amran Kaima.

Leave A Reply