Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Francis Alfred, amesema bodi itahakikisha wawekezaji wanaotumia fedha nyingi kujenga viwanda hawajikuti wakishindwa kuviendesha kutokana na uhaba wa korosho ghafi.
Amepongeza hatua ya NMB kuwakutanisha wadau hao, akisema ushirikiano kati ya taasisi za fedha na wafanyabiashara wa korosho ni muhimu katika kuongeza uzalishaji na kufanikisha azma ya nchi ya kupanua uwezo wa viwanda vya kubangua korosho ifikapo mwaka 2030.

Alfred pia amezitaka benki kuhakikisha malipo ya wakulima yanafanyika kwa wakati ili kuwawezesha kutimiza mahitaji yao ya kifedha na kujiandaa kwa shughuli zinazofuata za uzalishaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Biashara ya Kilimo kwa Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB, Christopher Mwalugenge, amesema benki hiyo imejipanga kusaidia biashara za korosho katika msimu wa 2026/2027 kupitia masuluhisho mbalimbali ya kifedha.
Amesema huduma hizo zinalenga kuwawezesha wanunuzi wa korosho kupitia minada na masoko ya awali kupata mitaji ya kununua mazao kwa wakati na kwa kiwango kinachohitajika, huku wabanguaji wakipata fedha za kununua malighafi za kuendesha viwanda vyao.
Mwalugenge amesema NMB pia inatoa masuluhisho ya kifedha yanayokidhi mahitaji ya wasafirishaji wa korosho nje ya nchi, ili kuwawezesha kufanya manunuzi kwa wakati na kutekeleza mikataba yao ya biashara katika masoko ya kimataifa.
Ameongeza kuwa benki hiyo imeimarisha huduma zake za malipo na miamala ili kurahisisha shughuli za biashara katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani wa korosho.
Kikao hicho kinatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za fedha na wadau wa korosho, hususan katika kuongeza upatikanaji wa mitaji, kuchochea ubanguaji wa korosho nchini na kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati.


