×

Serikali Yatangaza Nafasi 18 za Ajira Katika Taasisi Tano, Mwisho Kuomba Novemba 23

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (PSRS) imetangaza nafasi 18 za ajira katika taasisi tano za umma, ikiwemo Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (IAE), Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Tangazo hilo lenye kumbukumbu namba JA.9/16/01/63, la Novemba 10, 2026, limewataka Watanzania wenye sifa, uadilifu na uwezo wa kufanya kazi kuwasilisha maombi yao kupitia mfumo rasmi wa ajira serikalini.

Katika nafasi zilizotangazwa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaongoza kwa kuwa na nafasi 10 za Afisa Msaidizi wa Hali ya Hewa Daraja la II (Assistant Meteorological Officer II), zinazohitaji mwombaji kuwa na Stashahada ya Hali ya Hewa kutoka taasisi inayotambulika.

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) imetangaza nafasi tatu, zikiwemo nafasi mbili za Mkufunzi Daraja la II katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na nafasi moja ya Mkufunzi Daraja la II katika Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka.

Kwa upande wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (IAE), zimetangazwa nafasi mbili za Mhadhiri Msaidizi, moja katika fani ya Ujasiriamali na nyingine katika Elimu ya Watu Wazima.

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imetangaza nafasi moja ya Mkaguzi wa Usalama wa Mionzi Daraja la II katika fani ya Teknolojia ya Mionzi, huku Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kikiwa na nafasi mbili, moja ya Mkufunzi Daraja la II katika Uhandisi wa Umeme na nyingine ya Msaidizi wa Mafunzo katika Uhandisi wa Mitambo.

SIFA ZA WAOMBAJI

Kwa mujibu wa tangazo hilo, waombaji wote wanapaswa kuwa raia wa Tanzania na wasiwe na umri unaozidi miaka 45, huku nafasi za taasisi za kijeshi au zinazofuata taratibu za kijeshi zikiwa na masharti maalumu ya umri.

Waombaji wanatakiwa kuwasilisha nakala zilizothibitishwa za vyeti vya elimu kuanzia ngazi husika, nakala za matokeo ya masomo (transcripts), vyeti vya usajili wa kitaaluma pale inapohitajika pamoja na cheti cha kuzaliwa.

Pia, wanatakiwa kupakia picha ya hivi karibuni ya pasipoti katika mfumo wa maombi na kutaja wadhamini watatu wanaoaminika pamoja na mawasiliano yao.

Tangazo hilo limeeleza kuwa vyeti vya matokeo ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita visivyo rasmi (result slips), barua za utambulisho (testimonials) na nakala za matokeo zisizokamilika hazitapokelewa.

Aidha, watumishi walioajiriwa katika Utumishi wa Umma hawaruhusiwi kuomba nafasi hizo, huku wastaafu wa Utumishi wa Umma kwa sababu yoyote ile nao wakitakiwa kutoomba.

Waombaji wenye vyeti vya elimu vya nje ya nchi wanapaswa kuhakikisha vinatambuliwa na mamlaka husika, zikiwemo TCU, NECTA na NACTVET. Kwa nafasi zinazohitaji GPA, waombaji wanapaswa kuambatanisha cheti cha ukokotoaji wa GPA kutoka TCU.

NAMNA YA KUOMBA

Maombi yote yanapaswa kuwasilishwa kupitia mfumo wa Ajira Portal kwa kutumia anuani:

**https://portal.ajira.go.tz**

Mwombaji anatakiwa pia kuandika barua ya maombi iliyosainiwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza na kuiwasilisha kwa:

Secretary,

President’s Office – Public Service Recruitment Secretariat,

P.O. Box 2320,

Mahakama Street, Tambukareli,

Dodoma.

Mwisho wa kutuma maombi ni Novemba 23, 2026.

PSRS imesisitiza kuwa maombi yatakayowasilishwa kwa njia nyingine tofauti na mfumo rasmi hayatapokelewa, huku waombaji watakaokidhi vigezo pekee ndio watakaopata taarifa za hatua ya usaili.

Pia, imeonya kuwa uwasilishaji wa vyeti vya kughushi au taarifa za uongo utasababisha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

MWISHO

Mgawanyo wa nafasi 18

Taasisi

Nafasi

TMA

10

TLSB

3

IAE

2

TAEC

1

NIT

2

Jumla

18

Leave a Comment