×

Polisi Wamkamata Dereva Excavator kwa Kuharibu Mali za Mwajiri Kigamboni


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu wawili kwa tuhuma za makosa mbalimbali ya jinai, ikiwemo kuharibu mali za mwajiri kwa kutumia mashine ya kuchimba ardhi (Excavator) katika eneo la Mvumoni, Somangila, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa watuhumiwa hao ni Halidi Seleman Kalaghe, mwenye umri wa miaka 45, ambaye ni mwendesha mtambo wa Excavator. Anatuhumiwa kufanya uharibifu huo Novemba 10, 2026, majira ya saa 06:05 asubuhi, baada ya kutokea kwa mgogoro na mwajiri wake, kampuni ya China Energy Engineering Group Guanxi Hydroelectric Construction Bureau CO.LTD.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, mtuhumiwa huyo anadaiwa kutumia mtambo huo kuharibu maeneo mawili ya makazi pamoja na mali nyingine, ikiwemo gari aina ya Toyota Sienta lenye namba za usajili T 282 DEM, mali ya Brighton Abraham Mfangavo, gari la kubeba mafuta aina ya Sinotrack lenye namba T 391 EUN mali ya kampuni hiyo, nyumba tano na uzio.

Katika tukio jingine, Polisi wamekamata Peter Mmasi, mwenye umri wa miaka 32, mkazi wa Kimara, Dar es Salaam, kwa tuhuma za kumshambulia askari Polisi mwenye cheo cha Sajenti, Johnson Sylivery, aliyekuwa akimkamata. Mtuhumiwa huyo pia anatuhumiwa kutoa vitisho vya kumuua Carisma Amedeus Kileo, mkazi wa Kimara.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa taratibu za kisheria zinaendelea dhidi ya watuhumiwa hao ili hatua zaidi zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Leave a Comment