×

Mwigulu Atoa Onyo Kwa Wazazi Kuhusu Watoto Wanaoacha Shule Kwenda Machimboni

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanamaliza masomo na kuonya dhidi ya tabia ya wanafunzi kuacha shule na kwenda kufanya shughuli za uchimbaji madini.

Amesema elimu ni msingi muhimu utakaowawezesha vijana kujipatia kipato na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi hata baada ya shughuli za uchimbaji madini kukoma.

“Tusiache kuwapeleka shule watoto kwa sababu ya aina ya shughuli tunayofanya leo,” amesema Dkt. Mwigulu.

Waziri Mkuu ametoa wito huo Jumatano, Novemba 11, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika viwanja vya Segese, Jimbo la Msalala, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani humo.

Wito huo umefuatia maelezo ya Mbunge wa Msalala, Mabula Johnson Magangila, aliyebainisha kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikatisha masomo na kwenda machimboni, wakiwemo wanafunzi waliofaulu kwa daraja la kwanza na kuchaguliwa kuendelea na masomo.

Akizungumzia maisha yake ya utotoni, Dkt. Mwigulu alisimulia namna alivyokuwa akipenda kuchunga mifugo na kutokuwa tayari kwenda shule, hali iliyomfanya mwalimu wake kumshawishi baba yake amrudishe darasani.

Alinukuu maneno ya mwalimu huyo aliyekuwa akimhimiza baba yake kuhakikisha anapata nafasi ya kuendelea na elimu.

“Tuletee yule kijana alikuwa na akili mno. Tuletee aende shule,” alisema Dkt. Mwigulu akinukuu kauli ya mwalimu wake.

Alieleza kuwa elimu itawasaidia vijana kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, zikiwemo biashara ya madini ndani na nje ya nchi, badala ya kutegemea shughuli za uchimbaji pekee.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imepokea ombi la kuanzishwa kwa kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika eneo la Msalala, itakayotoa mafunzo yanayohusiana na sekta ya madini, na kwamba ombi hilo litafanyiwa kazi.

Hatua hiyo inalenga kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu na ujuzi katika sekta ya madini kwa wananchi wa eneo hilo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ameagiza usanifu wa barabara za kipaumbele mkoani Shinyanga ukamilishwe ili kuwezesha hatua zinazofuata za utekelezaji wa miradi hiyo.

Leave a Comment