×

Makamu wa Rais Ndejembi Atoa Onyo Kwa Wanaochakachua Pembejeo za Korosho – Picha

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ametoa onyo kwa maafisa ugani, maafisa kilimo na wafanyabiashara watakaobainika kuchakachua pembejeo za korosho na kuwanyonya wakulima, akisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayehusika na vitendo hivyo.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Novemba 12, 2026, Ndejembi amesema ruzuku ya pembejeo inayotolewa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha wakulima, hivyo haitaruhusiwa kutumiwa na watu wachache kujitajirisha.

Onyo hilo linakuja wakati uzalishaji wa korosho ukishuka kutoka tani 600,000 hadi tani 400,000, huku wakulima wakilalamikia ubora na ufanisi wa pembejeo wanazopatiwa.

Ndejembi ameitaka Wizara ya Kilimo kuchunguza malalamiko ya wakulima kuhusu ubora wa pembejeo, hususan salfa inayotumika kudhibiti visumbufu vya korosho, ikiwemo madai ya kuchakachuliwa au kupungua nguvu kutokana na kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

Amesema uzalishaji wa korosho ulikuwa tani 180,000 wakati Rais Samia anaingia madarakani, kabla ya kuongezeka hadi tani 600,000 kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali, ikiwemo utoaji wa ruzuku ya salfa.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema salfa ya unga haikutosheleza mahitaji katika msimu huu, hali iliyolazimu kuingizwa kwa salfa ya maji ambayo haikufanya vizuri katika baadhi ya maeneo. Amesema awali kulikuwa na takribani tani 16,000 za salfa ya unga, ambazo baadaye ziliongezwa kwa tani 10,000, lakini bado hazikukidhi mahitaji ya wakulima.

Chongolo amesema timu ya wataalamu kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Wizara ya Kilimo imepelekwa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha changamoto hiyo.

Ameongeza kuwa katika maandalizi ya msimu ujao, wizara inalenga kuhakikisha salfa ya unga inafikishwa katika maeneo ya uzalishaji ifikapo Machi 2027.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma za kijamii na miundombinu ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za uzalishaji katika mazingira salama na yenye amani.

Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi katika eneo la Mangaka, akieleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha sekta za kilimo, nishati, elimu, afya na miundombinu kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi.

Ameeleza kuwa Serikali tayari imetekeleza Mradi wa Maji wa Shilingi bilioni 38.4 katika Wilaya ya Nanyumbu, ambao umeanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

Aidha, akiwa katika ziara hiyo ya kikazi mkoani Mtwara, Ndejembi ametembelea kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, lililopo Lupaso, Wilaya ya Masasi, ambako alifanya maombi pamoja na familia ya marehemu, viongozi wa dini na viongozi wa Serikali, na kuweka shada la maua kwa heshima ya kiongozi huyo.

Leave a Comment