×

Waziri wa Hazina wa Marekani Ahamia Kambi ya Kijeshi Kufuatia Vitisho vya Iran

Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, ameripotiwa kuhamia kuishi katika kambi ya kijeshi pamoja na familia yake kufuatia kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu usalama wake kutokana na vitisho vinavyohusishwa na Iran.

Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, likinukuu vyanzo vinavyofahamu suala hilo, Bessent na familia yake wamechukua hatua hiyo kama tahadhari ya kiusalama kufuatia taarifa za kijasusi kuhusu uwezekano wa Iran kuwalenga maafisa wa Marekani.

Taarifa hiyo inafuatia onyo lililotolewa mwishoni mwa mwezi uliopita na afisa mkuu wa ujasusi katika utawala wa Rais Donald Trump, aliyedai kuwa Iran ilikuwa inaongeza juhudi za kuwalenga maafisa wa Marekani.

Hata hivyo, serikali ya Iran imewahi kukanusha madai kwamba inapanga kufanya mashambulizi dhidi ya maafisa au watu binafsi ndani ya Marekani.

Kwa upande mwingine, maafisa wa Marekani wameeleza kuwa uwezo wa Iran kutekeleza mashambulizi makubwa ndani ya Marekani au nje ya mipaka yake bado ni mdogo.

Kuhamia kwa Bessent katika kambi ya kijeshi kunaonesha kiwango cha tahadhari za kiusalama zinazochukuliwa na baadhi ya viongozi waandamizi wa Marekani wakati kukiwa na wasiwasi kuhusu vitisho vinavyohusishwa na Iran.

Leave a Comment