×

Rais Dkt. Mwinyi Afungua Kituo Cha Elimu Ya Anga, Kukuza Sayansi Na Ubunifu Kwa Vijana

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amefungua Kituo cha Elimu ya Anga cha Zanzibar Astronomy and Space Society (ZASS) na kuzindua Mradi wa Zanzibar Observatory and Planetarium, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo leo tarehe 14 Novemba 2026, Rais Dkt. Mwinyi amesema kituo hicho kitatoa fursa kwa vijana kujifunza sayansi ya anga kwa vitendo, kukuza vipaji, kufanya tafiti na kubuni teknolojia zitakazosaidia kutatua changamoto za jamii.

Amezielekeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu kushirikiana na ZASS kupanua elimu ya sayansi ya anga kwa wanafunzi wengi zaidi, huku akipendekeza kuanzishwa kwa kituo maalumu cha kuhifadhi historia ya Zanzibar katika Mradi wa Mercury wa NASA.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amekubali kuwa Mlezi wa ZASS, akitambua mchango wa taasisi hiyo katika kukuza sayansi na elimu ya anga nchini.


Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa ZASS, Amina Ahmad, amesema mradi huo unatarajiwa kuipa Zanzibar nafasi mpya katika sayansi na teknolojia ya anga kupitia kituo cha uchunguzi wa anga, ukumbi wa kidijitali wa maonesho na programu mbalimbali za elimu ya anga.

Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ametembelea mabanda ya wanafunzi kutoka skuli mbalimbali na kujionea ubunifu wao katika sayansi na teknolojia, kabla ya kukata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa kituo hicho.

Leave a Comment