×

China Yafanya Majaribio ya Kwanza ya Ndege ya Abiria Inayotumia Umeme Ikiwa na Marubani Ndani

BEIJING, CHINA: China imepiga hatua mpya katika teknolojia ya usafiri wa anga baada ya kampuni ya kutengeneza ndege ya Commercial Aircraft Corporation of China (COMAC) kufanikisha safari ya kwanza ya majaribio ya ndege yake ya abiria inayotumia umeme aina ya CE-25A ikiwa na marubani ndani.

Safari hiyo ilifanyika Novemba 14, 2026, katika mji wa Binzhou, jimbo la Shandong, mashariki mwa China, ikiwa ni hatua muhimu katika maendeleo ya teknolojia ya ndege zinazotumia nishati ya umeme.

Ndege hiyo ilibeba watu watatu, wakiwemo marubani wawili na mhandisi wa majaribio, na kukaa angani kwa dakika 16 na sekunde 38. Katika safari hiyo, iliruka umbali wa takribani kilomita 60.4 kabla ya kutua salama.

Kwa mujibu wa COMAC, safari hiyo iliendeshwa vizuri huku vipimo vyote vya utendaji wa ndege vikiwa ndani ya viwango vilivyotarajiwa.

Ndege ya CE-25A imeundwa kubeba abiria 19 na ina uzito wa juu wa tani 10 wakati wa kuruka.

Ina injini 10 ndogo zinazotumia umeme kuendesha feni maalumu zilizowekwa kwenye mabawa yake, tano kila upande.

Kwa mujibu wa taarifa za kiufundi za kampuni hiyo, ndege hiyo imeundwa kusafiri kwa kasi ya hadi kilomita 300 kwa saa na ina uwezo wa kufikia umbali wa kilomita 400 kwa safari moja.

ILIFANYA MAJARIBIO 19 KABLA YA KUBEBA WATU

Kabla ya safari yake ya kwanza ikiwa na watu ndani, CE-25A ilikuwa imekamilisha majaribio 19 ya kuruka bila rubani tangu ilipofanya safari yake ya kwanza ya kujiongoza Februari 2, 2026.

Mradi huo umeendelezwa kwa ushirikiano kati ya COMAC, kampuni ya kutengeneza betri ya CATL na Chuo Kikuu cha Shanghai Jiao Tong, pamoja na washirika wengine.

LENGO NI KUPUNGUZA GHARAMA ZA USAFIRI WA ANGA

Ndege hiyo inalenga zaidi kutoa huduma za safari fupi za kibiashara kati ya miji mbalimbali.

Matumizi ya umeme yanatarajiwa kupunguza utegemezi wa mafuta ya ndege, gharama za uendeshaji na uzalishaji wa hewa chafu unaotokana na injini wakati wa kuruka.

Hata hivyo, licha ya kufanikiwa kwa safari hiyo ya majaribio, CE-25A bado haijaanza kutoa huduma za usafirishaji wa abiria kibiashara.

Inatakiwa kwanza kukamilisha taratibu za uthibitishaji wa usalama na kupata kibali kutoka kwa mamlaka za usafiri wa anga nchini China.

Taarifa zinaeleza kuwa mamlaka hizo tayari zimepokea maombi ya COMAC ya kuidhinisha matumizi ya ndege hiyo.

Mafanikio hayo yanaongeza juhudi za China katika kuendeleza teknolojia mpya za usafiri wa anga, huku dunia ikiendelea kutafuta njia mbadala za kupunguza matumizi ya nishati ya mafuta katika sekta ya usafiri.

Leave a Comment