×

Isha Mashauzi Afunguka Urafiki Wake na Zuchu, Asema Ulianzia Kwa Mama Zao – Video

DAR ES SALAAM: Mkali wa muziki wa Taarab nchini, Isha Mashauzi, amefunguka kuhusu ukaribu wake na msanii wa Bongo Fleva, Zuchu, akieleza kuwa urafiki wao umetokana na uhusiano wa karibu uliokuwepo kati ya wazazi wao.

Isha amesema yeye na Zuchu si marafiki wa kawaida, bali wamekuwa karibu kutokana na historia ya upendo na urafiki wa mama zao ambao walikuwa pamoja katika kundi la TOT.

Akisimulia historia hiyo, Isha amesema marehemu mama yake na mama mzazi wa Zuchu walikuwa marafiki wakubwa kiasi kwamba hata waliposafiri kwa shughuli za muziki walikuwa wakilala sehemu moja.

Amesema ukaribu huo wa wazazi wao ndio uliojenga msingi wa uhusiano wao hadi sasa.

Isha amekumbushia pia namna Zuchu alivyomuunga mkono katika shoo yake ya kutimiza miaka 20 ya muziki iliyofanyika Super Dome, ambapo alimtafuta kwa simu na kumueleza dhamira yake ya kuhudhuria.

“Nakuja kukusapoti, niandalie meza,” alisema Zuchu katika simu hiyo, kwa mujibu wa simulizi ya Isha.

Isha amesema kitendo hicho kilimgusa sana na ni miongoni mwa ishara za upendo na urafiki ambazo hazisahauliki kirahisi.

SASA NI ZAMU YA MWANZA

Baada ya mafanikio ya shoo ya miaka 20 ya Isha Mashauzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam, safari ya kusherehekea safari yake ya muziki inaendelea kuelekea jijini Mwanza.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwapa mashabiki wa muziki wa Taarab jijini humo nafasi ya kushiriki katika shamrashamra za maadhimisho hayo na kushuhudia burudani kutoka kwa msanii huyo.

Urafiki wa Isha na Zuchu unaendelea kuwa sehemu ya simulizi inayogusa mashabiki, hasa kutokana na historia ya ukaribu wa familia zao ulioanzia kwa mama zao.

Leave a Comment