×

Watu 157 Wafungwa Jela Arusha, Mirungi Kg 123 na Bangi 1,020 Vyakamatwa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa mbalimbali wa makosa ya jinai, ambapo jumla ya watu 157 wamehukumiwa vifungo mbalimbali gerezani kuanzia Septemba 1, 2026 hadi Novemba 16, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 16, 2026 na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, waliohukumiwa wanahusishwa na makosa mbalimbali ikiwemo ubakaji, ulawiti, dawa za kulevya, kupatikana na nyara za serikali pamoja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika hukumu hizo, watuhumiwa wawili wamehukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya ubakaji, ulawiti na unyang’anyi wa kutumia silaha, huku mwingine akihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji.

Katika operesheni za kukabiliana na dawa za kulevya, Polisi wamewakamata watuhumiwa 39 waliokutwa na mirungi yenye uzito wa kilogramu 123, pamoja na watuhumiwa wengine 32 waliokuwa na misokoto 1,020 ya bangi.

Aidha, watuhumiwa 44 wamekamatwa wakiwa na pombe ya moshi yenye ujazo wa lita 190 pamoja na mitambo saba ya kutengeneza pombe hiyo haramu. Watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Katika operesheni nyingine, Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa saba kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali ambazo ni nyama za swala na pundamilia.

Hata hivyo, taarifa hiyo imeeleza kuwa Polisi Mkoa wa Arusha inaendelea na operesheni, doria na utoaji wa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Jimu Sanganyo, mkazi wa Kijiji cha Timbolo, Kata ya Sambasha, Wilaya ya Arumeru, kwa tuhuma za kumuua mke wake, Nanyori Jimu.

Tukio hilo limetokea Novemba 16, 2026 majira ya saa 9:00 usiku, ambapo mtuhumiwa anadaiwa kumuua mke wake kwa kumkata sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini mazingira yake na kuwezesha hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.

Leave a Comment