
ROMA, ITALIA – Papa Leo ameondoa hofu iliyokuwa imeibuka kuhusu hali yake ya kiafya baada ya kukamilisha ziara ya siku 12 katika nchi tatu za Amerika Kusini, licha ya kufanyiwa upasuaji wa saratani ya mapafu siku 24 tu kabla ya kuanza safari hiyo.
Papa huyo mwenye umri wa miaka 71 anatarajiwa kurejea Roma leo Jumanne, Novemba 17, 2026, baada ya kutekeleza ratiba iliyohusisha takribani shughuli 50 katika miji 10 ya Uruguay, Argentina na Peru.
Ziara hiyo ilikuwa miongoni mwa safari zenye ratiba nzito zaidi kuwahi kufanywa na kiongozi wa Kanisa Katoliki katika miongo kadhaa.

Papa Leo alisafiri umbali wa takribani kilomita 31,000, akihutubia waumini, kushiriki misa na mikutano mbalimbali, pamoja na kukutana na viongozi wa kijamii na kidini.
Hali yake ya kiafya ilikuwa imezua maswali kuhusu uwezo wake wa kuendelea na ratiba ya shughuli za kipapa baada ya madaktari kutangaza Oktoba 132026 kuwa alikuwa na saratani ya mapafu aina ya adenocarcinoma.
Hata hivyo, madaktari walieleza kuwa saratani hiyo ilikuwa imejikita katika eneo moja na haikuwa imesambaa, huku Papa huyo akitarajiwa kutohitaji matibabu mengine zaidi.
Kabla ya ziara hiyo, baadhi ya viongozi wa Vatican walikuwa wameeleza uwezekano wa Papa kupunguza shughuli zake za kimataifa kutokana na changamoto hiyo ya kiafya.

Katibu wa Jimbo la Vatican, Kardinali Pietro Parolin, aliwahi kusema huenda Papa akalazimika kurekebisha namna anavyoendesha kipindi chake cha uongozi.
Lakini kukamilika kwa ziara hiyo kumeibua mtazamo tofauti miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya Vatican.
John Thavis, mtaalamu wa masuala ya Vatican na mwandishi wa vitabu, alisema kukamilika kwa safari hiyo kama ilivyopangwa ni jambo linaloweza kuwapa matumaini Wakatoliki duniani kuhusu mwendelezo wa uongozi wa Papa.
Kwa upande wake, Elise Allen, mwandishi wa wasifu wa Papa Leo, alisema kiongozi huyo ameonyesha kiwango kikubwa cha nguvu na uvumilivu licha ya changamoto alizopitia kiafya.

Wakati wa ziara hiyo, Papa Leo alionekana kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali, akiwapungia mkono maelfu ya waumini waliokuwa wamejitokeza kumlaki na kutoa hotuba karibu 40 kwa sauti iliyoelezwa kuwa imara na yenye kueleweka.
Katika moja ya matukio makubwa, alikutana na takribani waumini milioni mbili katika eneo la ibada nchini Argentina Novemba 10.
Papa huyo pia alirejea katika mji wa Chiclayo, kaskazini mwa Peru, ambako aliwahi kuhudumu kama askofu kati ya mwaka 2015 na 2023.
Akizungumza wakati wa misa katika mji huo, alieleza kuwa changamoto ya kiafya aliyopitia ilikuwa kipindi kigumu cha majaribu ambacho alikuwa akikabiliana nacho.
Katika hotuba nyingine nchini Argentina, Papa Leo alisisitiza kuwa umri wala changamoto za kimwili havipaswi kuzima ari ya Mkristo katika kutekeleza imani yake.
Wachambuzi wa masuala ya Kanisa Katoliki wanaona ziara hiyo inaweza kuimarisha mwendelezo wa shughuli za Papa Leo, ambaye amekuwa na ratiba kubwa ya safari za kimataifa tangu kuchaguliwa kwake Mei 2025.
Hata hivyo, licha ya kukamilisha safari hiyo, mwenendo wa afya yake kwa muda mrefu utaendelea kuwa suala muhimu katika kutathmini ratiba na shughuli zake za baadaye.