×

Nafasi Mpya ya Kazi Yatangazwa Shirika la Posta, Maombi Mwisho Nov 30, 2026

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi moja ya kazi ya Meneja wa Kitengo cha Biashara za Kielektroniki (Manager – Electronic Business Section) katika Shirika la Posta Tanzania (TPC), ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utendaji na huduma za kidijitali katika shirika hilo.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa Novemba 17, 2026, nafasi hiyo inawalenga Watanzania wenye sifa za kitaaluma, uzoefu wa kutosha na uwezo wa kusimamia shughuli za biashara za kielektroniki.

Mwombaji anatakiwa kuwa na Shahada ya Uzamili au Stashahada ya Uzamili katika fani zinazohusiana na Teknolojia ya Habari, Sayansi ya Kompyuta, Uhandisi wa Kompyuta, Mawasiliano, Mifumo ya Habari, Usimamizi wa Biashara au fani nyingine zinazolingana kutoka katika taasisi inayotambulika.

Aidha, mwombaji anatakiwa kuwa na uzoefu wa kazi usiopungua miaka minane (8) na awe amewahi kushika nafasi ya juu katika eneo lake la kazi.

Majukumu ya meneja huyo yatakuwa ni pamoja na kusimamia na kukuza biashara kupitia mifumo ya kielektroniki, kuongeza mauzo ya huduma za mtandaoni, kuboresha mifumo ya malipo ya kidijitali pamoja na kuhakikisha wateja wanapata huduma bora kupitia majukwaa ya shirika hilo.

Pia, atahusika na kusimamia ushirikiano kati ya TPC na wadau wa huduma za kielektroniki, wakiwemo watoa huduma za malipo, kampuni za mawasiliano na washirika wengine wa kibiashara.

Kwa upande wa umri, waombaji wanatakiwa wasiwe na zaidi ya miaka 45, isipokuwa wale ambao tayari wapo katika Utumishi wa Umma.

Nafasi hiyo ni ya ajira ya kudumu na yenye mafao ya pensheni, huku mshahara ukiwa katika daraja la TPCSS 11 kwa mujibu wa viwango vilivyoidhinishwa na shirika hilo.

Katika masharti ya maombi, waombaji wanatakiwa kuwasilisha wasifu binafsi (CV) wenye mawasiliano sahihi, vyeti vya elimu vilivyothibitishwa, nakala za matokeo ya Kidato cha Nne na Sita, cheti cha kuzaliwa pamoja na picha ya pasipoti ya hivi karibuni.

Pia, kila mwombaji anatakiwa kutaja wadhamini watatu wanaoaminika na kuambatanisha mawasiliano yao.

Mwisho wa kutuma maombi ni Novemba 30, 2026, huku waombaji watakaopitishwa katika hatua ya awali ndio watakaopata taarifa za kushiriki usaili.

Tangazo hilo limetolewa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, likiwataka Watanzania wenye sifa zinazotakiwa kutumia fursa hiyo kuomba nafasi hiyo ya kazi.

Soma zaidi hapa >>NAFASI YA KAZI SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Leave a Comment