
Mchungaji mwenye uraia wa Marekani na Haiti, Christian Emmanuel Sanon, amepatikana na hatia ya mashtaka yote manane yanayohusiana na njama ya kumuondoa madarakani na kumuua aliyekuwa Rais wa Haiti, Jovenel Moïse, aliyeuawa mwaka 2021.
Sanon, mwenye umri wa miaka 67, alikutwa na hatia na mahakama ya shirikisho mjini Miami, Florida, nchini Marekani, baada ya kesi iliyodumu kwa wiki nane.
Anakabiliwa na uwezekano wa kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kutokana na makosa hayo, yakiwemo kula njama ya kumuua au kumteka nyara mtu.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, Sanon alikuwa na azma ya kushika madaraka ya urais wa Haiti baada ya kuondolewa kwa Moïse, huku akituhumiwa kupanga mapinduzi hayo kwa kushirikiana na watu wengine.
Inadaiwa kuwa mpango huo ulihusisha shambulio la kutumia silaha katika makazi ya rais yaliyopo Port-au-Prince, mji mkuu wa Haiti, na kwamba Sanon alitarajia kupata nafasi ya urais ili kutoa mikataba mikubwa ya serikali kwa kampuni za ulinzi zenye makao yake Florida.
Kampuni zilizotajwa katika mpango huo ni Counter Terrorist Unit Federal Academy na Counter Terrorist Unit Security, ambazo kwa pamoja zilijulikana kama CTU.
Waendesha mashtaka wamedai kampuni hizo zilitarajiwa kusaidia kufadhili mapinduzi hayo kwa matarajio ya kupata mikataba ya serikali iliyohusisha miradi ya miundombinu, vifaa vya usalama na huduma za ulinzi.
Hata hivyo, wakili wa Sanon amesema mteja wake bado anasisitiza kuwa hana hatia na anakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Mauaji ya Rais Moïse yalitokea Julai 2021, wakati watu wenye silaha walipovamia makazi yake mjini Port-au-Prince na kumuua. Mke wake, Martine Moïse, naye alijeruhiwa katika shambulio hilo.
Kifo cha Moïse kiliiacha Haiti katika kipindi kigumu cha kisiasa, huku kukosekana kwa uongozi thabiti kukichangia kuongezeka kwa ukosefu wa usalama na machafuko yanayohusishwa na magenge ya uhalifu.
Wakati huo huo, Martine Moïse ametangaza nia yake ya kuwania urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027, hatua inayofungua ukurasa mwingine wa ushindani wa kisiasa nchini humo.