Benki ya Stanbic Tanzania imeshiriki Mbio za Hisani za TPDC Marathon 2026, zilizoandaliwa chini ya kaulimbiu “Hatua Yako, Okoa Maisha”, kwa lengo la kuchangisha fedha za kugharamia upasuaji wa moyo kwa watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Stanbic imetoa mchango wa shilingi milioni 50, ikiwa sehemu ya fedha zilizochangishwa kupitia mbio hizo, ambazo zimefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi milioni 500, na kuvuka lengo la awali la shilingi milioni 200.
Akizungumza baada ya mbio hizo leo jijini Dar es Salaam, Mgeni Rasmi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, ameipongeza Stanbic, pamoja na wadhamini na washiriki wengine kwa kuunga mkono juhudi za TPDC na kuchangia kufanikisha matibabu ya watoto wenye changamoto za moyo.
Ushiriki wa Stanbic uliongozwa na Mkuu wa Wateja Binafsi na Wateja Maalum, Omari Mtiga, pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo waliojitokeza kuungana na washiriki wengine katika kuunga mkono lengo hilo la kuokoa maisha ya watoto.
Akizungumza baada ya mbio hizo, Omari amesema: “Mchango huu unaendeleza dhamira ya Stanbic ya kuboresha afya na ustawi wa jamii. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Stanbic imetoa shilingi milioni 320 kupitia JKCI kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo, hususan kutoka familia zenye kipato cha chini na maeneo ya vijijini, kwa lengo la kusaidia watoto 20 kila mwaka.”