
ABUJA, NIGERIA: Lugha ya Kiswahili imeidhinishwa kuwa mojawapo ya lugha rasmi za Shirikisho la Kandanda Afrika (CAF), kufuatia mabadiliko yaliyofanywa katika Katiba ya shirikisho hilo.
Uamuzi huo umetangazwa na Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, baada ya kupitishwa kwa kura nyingi na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 48 wa CAF uliofanyika jijini Abuja, Nigeria.
Kwa hatua hiyo, Kiswahili kinaungana na lugha nyingine nne ambazo ni Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu na Kireno, na kufanya jumla ya lugha rasmi za CAF kufikia tano.
Lugha hizo zitatumika katika shughuli mbalimbali za shirikisho hilo, zikiwemo mikutano na matukio yanayoandaliwa na CAF.
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Motsepe ameipongeza Tanzania, Kenya na Uganda kwa mchango wao katika kuhakikisha Kiswahili kinapata hadhi hiyo, akieleza kuwa hatua hiyo ni fursa muhimu kwa maendeleo ya Afrika.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Tanzania na Afrika Mashariki zimeupokea uamuzi huo kwa heshima kubwa.
Msigwa, aliyemwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Tanzania itatumia fursa hiyo kukuza Kiswahili na utamaduni wa Mswahili katika majukwaa ya kimataifa.
Akiwa ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Selestine Kakele, pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, Msigwa ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia mchakato wa kuiomba CAF kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi miaka mitatu iliyopita.
Amesema mafanikio hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha nafasi ya Kiswahili barani Afrika na kuongeza fursa za lugha hiyo kutumika katika shughuli za kimataifa, hususan katika michezo.
Uamuzi huo unatarajiwa kuongeza mwonekano wa Kiswahili katika majukwaa ya soka barani Afrika na kuimarisha nafasi yake kama lugha inayounganisha watu wa mataifa mbalimbali.
