
Maafisa wa Ujasusi wa Jeshi la Israel (IDF) wamemuonya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuwa mpango wowote wa kuishambulia Iran unaweza kusababisha vita vikubwa vya kikanda vitakavyohusisha mataifa na maeneo mbalimbali, yakiwemo Lebanon, Syria na Gaza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Channel 12 nchini Israel, onyo hilo lilitolewa wiki iliyopita katika kikao cha faragha kilichowahusisha Netanyahu na maafisa waandamizi wa ulinzi, wakati serikali ikiendelea kutathmini uwezekano wa kufanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran.
Tathmini ya ujasusi wa kijeshi inaeleza kuwa shambulizi dhidi ya Iran linaweza kufungua mapambano katika nyanja nyingi za kijeshi, tofauti na matarajio ya baadhi ya viongozi wa Israel waliodhani kuwa operesheni hiyo ingeweza kudumu kati ya siku tatu hadi tano pekee.
Wakati huo huo, mwanasiasa wa upinzani nchini Israel, Avigdor Liberman, ameonya dhidi ya kuishambulia Iran kwa sasa, akidai kuwa hatua hiyo inaweza kuchochewa na maslahi ya kisiasa badala ya sababu za kiusalama.
Kwa upande mwingine, shirika la utangazaji la Kan limeripoti kuwa Netanyahu anafanya juhudi za kumshawishi Rais wa Marekani, Donald Trump, kuishambulia Iran haraka iwezekanavyo.
Hata hivyo, Trump bado hajafanya uamuzi wa mwisho kuhusu uwezekano wa kuanzisha mashambulizi mapya, huku baadhi ya maafisa wa Ikulu ya Marekani wakipendelea kuipa muda zaidi Iran kutokana na athari za vita vilivyopita na vikwazo vya kiuchumi vinavyoikabili nchi hiyo.
Akizungumza na Fox News Jumapili, Trump alisema anaelekea kuunga mkono mashambulizi mengine dhidi ya Iran iwapo makubaliano hayatapatikana kabla ya mwaka mpya.
Trump pia aliishutumu Iran kwa kuchelewesha mazungumzo ya kufikia makubaliano huku ikiendelea kuonesha kile alichokitaja kuwa mwenendo wa uchokozi.
Katika hatua nyingine, Iran imeanza kutekeleza mgao wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini humo kutokana na changamoto za uzalishaji wa nishati na uharibifu wa miundombinu.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amewataka wananchi na taasisi za serikali kupunguza matumizi ya umeme ili kuhakikisha uzalishaji na usambazaji wa nishati vinaendelea.
Kwa mujibu wa mamlaka za nishati nchini humo, baadhi ya maeneo yanatarajiwa kukabiliwa na mgao wa umeme wa takribani saa mbili kila baada ya siku mbili, huku maeneo mengine yakikabiliwa na mgao wa kila siku.
Pezeshkian amesema mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya miundombinu ya nishati ya Iran yameongeza changamoto zilizokuwepo, hasa wakati nchi hiyo ikijiandaa kukabiliana na mahitaji makubwa ya nishati katika kipindi cha majira ya baridi.
Hali hiyo inaendelea kuongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa kurejea kwa mapigano makubwa kati ya Iran, Israel na Marekani, huku juhudi za kidiplomasia zikisubiriwa kuamua mwelekeo wa mgogoro huo.